Sep 19, 2023 13:04 UTC
  • Maporomoko ya ardhi kaskazini-magharibi mwa DR Congo yaua takriban watu 17

Watu wasiopungua 17 wamepoteza maisha Kaskazini Magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kufuatia maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa. Viongozi wa eneo hilo wamesema idadi ya watu waliofariki dunia inaweza kuongezeka huku waokoaji wakiendelea na jitihada za kupekua vifusi vya nyumba zilizoporomoka.

Maafa hayo yalitokea siku ya Jumapili kando ya Mto Congo katika mji wa Lisal,  jimbo la Mongala. Kwa mujibu wa Matthieu Mole, mkuu wa shirika  la Forces Vives, waathiriwa hao walikuwa wakiishi katika nyumba zilizojengwa chini ya mlima.

Mashirika ya kiraia ya Congo yalihusisha tukio hili na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika eneo hili.

Idadi ya waathirika inatarajiwa kuongezeka kwa kuzingatia  kwamba miili ya walioaga dunia bado iko chini ya vifusi.

Gavana Cesar Limbaya Mbangisa amesema, zana za kisasa zinahitajika ili kusaidia jitihada za kuondoa vifusi na kuokoa walionusurika. Gavana huo pia ametangaza siku tatu za maombolezo katika jimbo hilo.

Wataalamu wa hali ya hewa wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa, umaskini na miundo mbinu duni katika maeneo hayo unawaweka hatarini zaidi wakazi wake katika kukabiliana na hali mbaya ya hewa kama vile mvua kubwa zinazonyesha mara kwa mara barani Afrika.

Mwezi Aprili Rais Felix Tshisekedi alitangaza siku ya maombelezi kufuatia kufariki dunia watu 16 katika maporomoko ya ardhi yaliyotokea katika eneo la Lubero kaskazini mwa mkoa wa Kivu.