Oct 15, 2023 11:28 UTC
  • Wakenya wawasha mishumaa kuonyesha mshikamano na Wapalestina

Wananchi wa Kenya wamekusanyika na kuwawasha mishumaa katika mji mkuu wa nchi hiyo, Nairobi kuonyesha mshikamano wao na wananchi wa Palestina. Mashirika yaliyoandaa shughuli hiyo ni pamoja na Kenyans 4 Palestine, The Pan African Palestine Solidarity Network (PAPSN) na podkasti ya 'Until Everyone is Free.'

Washiriki wa shughuli hiyo iliyofanyika jana Jumamosi walisisitizia haja ya kukomeshwa ukatili na uhalifu unaofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. Mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika maeneo yenye wakazi wengi wa Ukanda huo yamesababisha Wapalestina 2,215 kuuawa shahidi na wengine 8,714 kujeruhiwa.

Aisha Ahmed, mmoja wa washiriki amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu akisema kuwa, "Inavunja moyo kuona watu wasio na hatia wanauawa kila siku na mabomu yanayodondoshwa na droni za Israel."

Ameitaka dunia ichukue hatua za kivitendo kukomesha msururu huo wa vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa wananchi wa Palestina katika Ukanda wa Gaza hasa watoto na wanawake.

Ahmed Ibrahim, mwanachama wa vuguvugu la 'Kenyans 4 Palestine' ambaye pia alishiriki kikao hicho cha amani cha kuwatetea Wapalestina amesema: Lengo letu ni kutoa hamasa juu ya mgogoro unaoendelea na masaibu na dhiki wanazopitia Wapalestina.

Wananchi wa Kenya walioshiriki shughuli hiyo mbali na kutangaza uungaji mkono wao kwa watu wa Palestina, wameulaani vikali utawala haramu wa Israel kwa kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Juzi Ijumaa, wananchi wa Afrika Kusini walifanya maandamano kwa mara nyingine tena wakionyesha mshikamano wao na watu wanaodhulumiwa wa Palestina na kutangaza uungaji mkono wao kwa mapambano ya ukombozi wa Palestina.

Tags