Oct 18, 2023 03:50 UTC
  • UNHCR: Watu elfu nne wameuliwa Darfur, Sudan, mali za raia zimeharibiwa

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema, watu wapatao 4,000 wameuawa huku mali za raia zikiharibiwa katika mapigano yanayoendelea huko jimboni Darfur nchini Sudan, mapigano ambayo yalianzia kwenye mji mkuu Khartoum miezi sita iliyopita na kusambaa hadi nje ya mji huo, kati ya Jeshi la Serikali (SAF) na wanamgambo wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF).

Msemaji wa UNHCR Eujin Byun amewaeleza waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kwamba kuongezeka kwa vifo na ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya raia wasio na hatia, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa wakimbizi wa ndani, kumeshuhudiwa katika kipindi hiki cha miezi sita tangu kuanza kwa mzozo huo nchini Sudan.

Kulingana na ripoti mpya ya UNHCR iliyotolewa hivi karibuni, takribani  raia 4,000 wameuawa na wengine 8,400 wamejeruhiwa jimboni Darfur pekee kati ya Aprili 15 na mwisho wa mwezi Agosti, huku wengi wao wakilengwa kutokana na sababu za kabila, hasa  jimboni  Darfur Magharibi.

Watoto waliokimbia makazi yao wamenaswa katika mapigano na kuuawa au kutiwa ulemavu huku skuli zao zikiharibiwa kwa makombora; na wale ambao wamefika maeneo salama wanakabiliana na changamoto ya kisaikolojia. 

Takriban miji na vijiji 29 vimeharibiwa kote Darfur baada ya uporaji, uchomaji moto na ufyatulianaji risasi kiholela wa makombora makubwa katika kambi na maeneo ya mikusanyiko ya watu waliohamishwa na kusababisha vifo vya mamia ya watu.

Bujin amesema, "raia wanaojaribu kukimbia Darfur ili kutafuta usalama inaripotiwa kuwa wanazuiwa kufanya hivyo au wanakabiliwa na changamoto kwenye vizuizi, wanakamatwa na kuswekwa korokoroni."

Wakati huohuo, Shirika hilo la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi limezitolea mwito pande hasimu nchini Sudan ziache mapigano na kuheshimu sheria za kimataifa za kibinadamu na haki za binadamu.../

 

Tags