Nov 28, 2023 06:17 UTC
  • Algeria kuwa mwenyeji wa mkutano wa kujadili njia za kuishtaki Israel ICC

Algeria imejiunga na orodha ya nchi zinazotaka kufanyike uchunguzi kuhusiana na jinai za kivita zilizofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza, na kushtakiwa utawala haramu katika vyombo vya kimataifa.

Tayari Karim Khan, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC amepokea maombi kutoka kwa nchi tano (Afrika Kusini, Bangladesh, Bolivia, Comoro na Djibouti) ya kutakiwa kuchunguza jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza.

Shirika la habari la IRNA limemnukuu Ibrahim Tairi, Mkuu wa Chama cha Taifa cha Mawakili Algeria akisema nchi hiyo itakuwa mwenyeji wa mkutano wa kujadili njia za kuuchunguza na kuushtakia utawala wa Kizayuni ICC na katika mahakama nyingine za kimataifa.

Tairi amesema mkutano huo wa kimataifa wa siku mbili utakaoanza kesho Novemba 29, utawaleta pamoja wataalamu wa sheria kutoka nchi mbalimbali za Kiarabu na Ulaya.

Kabla ya hapo, Rais wa Algeria alitoa mwito wa kushtakiwa Israel ICC na kusisitiza kwamba, utawala ghasibu haujali wala kuheshimu maamuzi ya taasisi muhimu za kimataifa kama Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mauaji ya watoto wa Kipalestina huko Gaza

Rais Abdelmadjid Tebboune alisisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni hautilii maanani hata kidogo Umoja wa Mataifa na unapuuza yale yanayoidhinishwa na taasisi hiyo na kukiuka wajibu na majukumu yake.

Kadhalika mapema mwezi huu, Bunge la Algeria lilipasisha sheria ambayo inamruhusu Rais wa nchi kama ikilazimu kuingia vitani na utawala ghasibu wa Israel kwa ajili ya kuwatetea wananchi wasio na hatia wa Palestina.

Algeria ambayo ni miongoni mwa mataifa ambayo yamekuwa mstari wa mbele kupaza sauti kuliunga mkono taifa la Palestina na kulaani jinai za Israel dhidi ya wananchi hao madhulumu.

 

 

Tags