Dec 03, 2023 10:42 UTC
  • Wanigeria waandamana wakitaka kukatwa uhusiano na Israel

Kwa mara nyingine tena, maelfu ya Waislamu na waungaji mkono wa Palestina katika mji wa Kano, kaskazini mwa Nigeria wameandamana na kulaani jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina hasa wa Ukanda wa Gaza.

Shirika la habari la Iran Press limeripoti habari hiyo na kueleza kuwa, viongozi wa Kiislamu, wanaharakati wa haki za binadamu na baadhi ya wanasiasa wa Nigeria walioshiriki katika maandamano hayo ya jana Jumamosi katika mji Kano, wametoa mwito kwa Rais Bola Ahmad Tinubu wa nchi hiyo kukata uhusiano baina ya taifa hilo na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba bendera za Palestina na picha zinazoshiria ukatili wa Israel katika  Ukanda wa Gaza, wamesisitiza juu ya ulazima wa kukomesha mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa ukanda huo, yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni.

Washiriki wa maandamano hayo dhidi ya Wazayuni walikuwa wamebeba mabango yaliyosomeka: "Serikali ya Nigeria lazima ikate uhusiano na utawala wa Israel," "Kano inasimama na Palestina," "Mauti kwa Israel," na "Sisi sote ni Wapalestina." 

Malama Rabi Muhammad, mwanachuoni wa kike wa Kiislamu aliyeshiriki maandamano hayo amenukuliwa na Iran Press akisema kuwa, "Kama unavyoona, watu wa matabaka mbalimbali wamejitokeza kuiunga mkono Palestina. Iwapo serikali ya Nigeria ni ya kidemokrasia kikweli, inapasa kuheshimu matakwa ya taifa na kukata uhusiano na Israel."

Waislamu nchini Nigeria wamekuwa wakiandamana kila mara na kusisitiza uungaji mkono wao mkubwa kwa wananchi wa Palestina na muqawama wao dhidi ya uvamizi wa Israel na jinai zake.

Kabla ya hapo pia, Waislamu katika jimbo hilo la Kano, na pia Jimbo la Bauchi walifanya maandamano wakipeperusha bendera za Palestina huku wakitoa nara za "Tunaunga mkono Hamas," "Tunaunga mkono Palestina," "Mauti kwa Israel na Mauti kwa Marekani".

Tags