Dec 29, 2023 02:29 UTC
  • Kiongozi wa RSF yuko Addis Ababa baada ya kushindwa kukutana na Al-Burhan

Kamanda wa wapiganaji wa Kikosi cha Msaada wa Haraka kinachopigana na jeshi la Sudan, Luteni Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, aliwasili katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa, jana Alhamisi baada ya kutembelea Uganda na kukutana na Rais Yoweri Museveni.

Luteni Jenerali Hamdan Dagalo alipokewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Bole na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Demeke Mekonnen, katika kile kinachoonekana kuwa ni jitihada za kikanda za kutatua mzozo wa ndani nchini Sudan.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Sudan (SUNA), Mkuu wa Baraza la Utawala wa Mpito wa Sudan, Luteni Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan, alitazamiwa kukutana na Jenerali Dagalo jana, Alhamisi, nchini Djibouti, lakini mkutano huo uliahirishwa.

SUNA imetangaza kuwa, “Serikali ya Sudan imeeleza masikitiko yake kutokana na mienendo ya wanamgambo waasi wa RSF ya kuacha kusikiliza sauti ya akili na mantiki, na kutokuwa tayari kusitisha uharibifu wa Sudan na watu wake, na hili limedhihiri kutokana na kutoitikia mwito wa kuhudhuria mkutano Djibouti.”

Kwa upande wake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan imetangaza kwamba imepokea risala kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Jamhuri ya Djibouti, na kusema kuwa kamanda wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) Luteni Jenerali Hamdan Dagalo, hakuweza kufika Djibouti kwa ajili ya mkutano huo kwa sababu za kiufundi.

Taarifa ya Wizara hiyo imeongeza kwamba uratibu utafanywa tena ili kuzikutanisha pande hizo mbili mwezi ujao.

Majenerali al Burhan na Dagalo

Dagalo amewasili Ethiopia baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, siku ya Jumatano iliyopita katika ziara ya kwanza ya nje iliyotangazwa tangu kuzuka kwa mapigano kati ya Vikosi vya Msaada wa Haraka na jeshi la Sudan Aprili mwaka huu.

Maelfu ya watu wameuawa na mamilioni ya wengine wamelazimishwa kuwa wakimbizi ndani na nje ya Sudan kutokana na vita vya kuwania madaraka kati ya majenerali wawili waitifaki wa zamani, Luteni Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan na Luteni Jenerali Hamdan Dagalo.

Tags