Jul 07, 2016 14:06 UTC
  • Askari 12 wa Libya wauawa katika hujuma ya bomu Benghazi

Kwa akali askari 12 wa jeshi la Libya wameuawa katika shambulizi la bomu la kutegwa garini katika mji wa Benghazi, mashariki mwa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Habari zinasema kuwa, hujuma hiyo ya bomu ilitokea jana katika kambi ya jeshi katika wilaya ya Kafur, magharibi mwa mji wa Benghazi na kusababisha vifo vya wanajeshi 12 wa Libya na wengine 35 kujeruhiwa. Mohamed al-Azoumi, msemaji wa jeshi la Libya amesema maafisa wawili wa ngazi za juu wa jeshi la nchi hiyo wameuawa katika hujuma hiyo ingawaje hakuna kundi lolote la kigaidi limekiri kuhusika nalo hadi tunaenda mitamboni.

Shambulizi hilo limefanyika wiki moja baada ya watu 14 kuuawa katika mapigano makali kati ya jeshi la Libya na wanachama wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika mji wa Sirte. Aidha limejiri siku chache baada ya Ahmed al Mismari, msemaji wa vikosi vya ulinzi vya Libya kutangaza habari ya kukombolewa eneo la Garyounis la mjini Benghazi, kaskazini magharibi mwa Libya.

Tags