Feb 07, 2024 03:49 UTC
  • Kiongozi wa tapo la kidini Kenya na wenzake 29 washtakiwa kwa mauaji ya watoto 121

Kiongozi wa tapo la kidini nchini Kenya liitwalo Good News International, Paul Nthenge Mackenzie na wasaidizi wake 29 wameshtakiwa rasmi kuhusika na mauaji ya watoto 191 ambao miili yao ilipatikana kati ya mamia ya watu waliozikwa kwenye msitu wa Shakahola.

Hata hivyo Mackenzie na wenzake wote walikana mashtaka yaliyowasilishwa mbele ya mahakama katika mji wa Malindi hapo jana Jumanne.
Mshtakiwa mmoja ameonekana kuwa hana uwezo wa kiakili kujibu mashtaka na ameagizwa kurejeshwa katika Mahakama Kuu ya Malindi baada ya mwezi mmoja.
 
Waendesha mashtaka walisema Mackenzie aliamuru wafuasi wake wajiue kwa njaa wao na watoto wao ili waweze kwenda mbinguni kabla ya ulimwengu kuisha, katika mojawapo ya maafa mabaya zaidi yanayohusiana na masuala ya ibada katika historia ya karibuni.
Maiti zikifukuliwa kwenye msitu wa Shakahola

Paul Mackenzie, ambaye ni dereva wa zamani wa teksi aliyejiita mchungaji tayari amefunguliwa mashtaka ya "ugaidi", mauaji ya bila kukusudia pamoja na kutesa watoto na ukatili. Alikamatwa Aprili mwaka jana baada ya miili kupatikana katika msitu wa Shakahola.

Uchunguzi wa maiti ulionyesha kuwa wengi wa wahasiriwa 429 walikufa kwa njaa. Lakini wengine, ukijumuisha na watoto, walionekana kunyongwa, kupigwa, au kukosa hewa.

Kesi hiyo, iliyopewa jina la "Mauaji ya Msitu wa Shakahola", ilipelekea serikali ya Kenya kulipa zingatio maalumu suala la kuwepo udhibiti mkali wa shughuli za madhehebu tofauti za kidini.

Likiwa ni taifa lenye Wakristo wengi, Kenya imetatizika kudhibiti makanisa na matapo yasiyofaa ambayo yanajihusisha na uhalifu.../

 

Tags