Feb 07, 2024 06:04 UTC
  • Milipuko iliyotokea sokoni Mogadishu yauwa watu 10 na kujeruhi wengine 20

Takriban watu 10 waliuawa jana baada ya milipuko kadhaa kutokea katika soko lililokuwa na msongamano mkubwa wa watu huko Mogadishu, mji mkuu wa Somalia.

Milipuko hiyo ilitokea katika soko kubwa la Bakara huko Mogadishu. Wauguzi watatu katika hopistali ya Erdogan huko Mogadishu wameliambia shirika la habari la Reuters kuwa watu zaidi ya 20 waliojeruhiwa katika milipuko hiyo walifikishwa hospitalini hapo kwa ajili ya matibabu. 

Mohamed Ali mfanyabiashara katika soko hilo la Bakara ambaye amesema alisaidia kuwabeba watu waliopoteza maisha na nmajeruhi katika milipuko hiyo ameiambia televisheni ya al Jazeera kuwa walisikia milipuko minne mikubwa ndani ya maduka manne mashuhuri yanayouza vifaa vya kielektroniki na kupigwa na butwaa. 

Polisi ya Somalia imetangaza kuwa uchunguzi tayari umeanza kuhusiana na milipuko hiyo ya jana huko Mogadishu. Chanzo cha milipuko hiyo hadi sasa bado hakijafahamika ingawa kundi la kigaidi la al Shabaab lenye mfungamano na  mtandao wa kiqaidi wa Al Qaida mara kwa mara limekuwa likifanya mashambulizi ya ulipuaji mabomu katika maeneo yenye watu wengi huko Somalia. 

Wanamgambo wa al Shabab wa nchini Somalia 

Bakara, soko kubwa zaidi la Mogadishu limejaa wafanyabiashara mbalimbali na ni sehemu ambayo wananchi wengi hununua vyakula vyao, nguo, dawa, vifaa vya elektroniki na bidhaa nyingine mbalimbali za mahitaji kila siku.

Tags