Feb 11, 2024 12:07 UTC
  • Le Monde: Hakuna matumaini ya kukomeshwa vita hivi karibuni nchini Sudan

Ripoti iliyochapishwa na gazeti la Ufaransa la Le Monde imesema kwamba, baada ya zaidi ya miezi 9 ya vita kati ya Jeshi la Sudan linaloongozwa na Abdel Fattah al-Burhan na Vikosi vya Msaada wa Haraka chini ya uongozi wa Mohamed Hamdan Dagalo, hakuna uwezekano wa kumalizika vita hivyo karibuni.

Ripoti ya gazeti hilo imeeleza kwamba, mashirika yote ya misaada ya kibinadamu yanayofanya kazi nchini Sudan yamepiga kengele ya hatari kuhusu hali mbaya inayoshuhudiwa sasa nchini humo; kwani wakati karibu watu milioni 8 wakiwa wakimbizi kutokana na mapigano, ikiwa ni pamoja na Wasudani milioni moja waliokimbilia nchi jirani, mzozo wa nchi hiyo sasa unatambuliwa kuwa janga kubwa zaidi la watu kuhama makwao duniani, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.

Nusu ya idadi ya watu milioni 44 pia wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, na mgogoro huo tayari umesababisha vifo vya makumi ya maelfu ya watu na kujeruhiwa maelfu ya wengine.

Hadi sasa juhudi za kikanda na za kimataifa za kutafuta suluhisho la kisiasa la vita vya ndani nchini Sudan zimeambulia patupu. 

Maelfu ya Wasudani wanasumbuliwa na njaa

Majuzi, Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa, mkuu wa jeshi nchini Sudan, Jenerali Abdel-Fattah al-Burhan na mpinzani wake ambaye ni kamanda wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF), Mohamed Hamdan Dagalo, wamekubali kukutana kwa ajili ya mazungumzo kuhusu hali mbaya ya binadamu nchini humo.

Mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia misaada ya binadamu Martin Griffiths amesema kuwa, siku chache zilizopita alizungumza na viongozi hao wawili lakini haijathibitishwa ni lini na wapi mazungumzo hayo yatafanyika.

Hata hivyo Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Sudan Alhamisi iliyopita ilikanusha taarifa iliyotolewa na Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa, Martin Griffiths, ambaye alidokeza kuwa Jenerali Abdel Fattah Al-Burhan, amekubali kukutana na Kamanda wa Kikosi cha Msaada wa Haraka, Mohamed Hamdan Dagalo (Hemedti), kwa madhumuni ya kuwezesha kuwasili kwa misaada kwa watu walioathirika na vita huko Sudan.

Tags