Feb 28, 2024 06:48 UTC
  • Morocco: Gaza inashuhudia janga la kuogofya la kibinadamu

Waziri wa Mambo ya Nje wa Morocco amesema Wapalestina wa Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na 'janga la kibinadamu' wakati huu ambapo utawala wa Kizayuni wa Israel umeshadidisha mashambulizi yake ya kinyama dhidi ya eneo hilo lililozingirwa.

Nasser Bourita alisema hayo jana Jumanne katika mkutano wa 55 wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi na kuongeza kuwa, "Gaza inapitia mgogoro ambao haujawahi kushuhudiwa na janga la kibinadamu ambalo jamii ya kimataifa haipasi kuendelea kufumbia macho."

Bourita ameeleza bayana kuwa, kuna udharura wa kutekelezwa mara moja usitishaji vita wa kudumu katika Ukanda wa Gaza. Aidha ametaka kulindwa raia wa eneo hilo, sambamba na kufikishiwa misaada ya kutosha ya kibinadamu.

Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Morocco licha ya kushutumu rasmi kile ilichokiita "ukiukaji wa wazi wa vifungu vya sheria za kimataifa" uliofanywa na Israel katika vita vyake dhidi ya Gaza, lakini haijaonyesha ishara yoyote ya kubadilisha msimamo iliochukua wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel ambao umelaaniwa na kukosolewa vikali katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Wamorocco katika maandamano ya kuonyesha mshikamano na Wapalestina

Maelfu ya wananchi wa Morocco wamekuwa wakifanya maandamano ya mara kwa mara katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na kulaani jinai zinazoendelea kufanywa na jeshi la Israel huko Gaza.

Waandamanaji nchini Morocco wamelaani ukatili wa utawala wa Kizayuni wa kuwatesa kwa njaa, kuwazingira kila upande na kujaribu kuwahamisha kwa nguvu watu wa Ukanda wa Ghaza.

Kadhalika wananchi wa Moroco wanaishinikiza pia serikali ya Rabat kufuta makubaliano ya kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala katili wa Israel.

Tags