Mar 06, 2024 07:42 UTC
  • Sudan karibuni itakumbwa na janga kubwa la njaa

Mpango wa Chakula Duniani (WFP) leo umetahadharisha kuwa vita vya Sudan vilivyodumu kwa takriban miezi 11 kati ya majenerali hasimu vinahatarisha nchi hiyo kuathiriwa na janga kubwa la njaa.

Cindy McCain Mkurugenzi Mtendaji wa WFP ameeleza kuwa mamilioni ya maisha ya watu na amani na uthabiti wa eneo zima vinakabiliwa na hatari hivi sasa. Amesema, miaka 22 iliyopita jimbo la Darfur magharibi mwa Sudan lilikuwa eneo lililoathiriwa na maafa makubwa zaidi ya njaa duniani na dunia ilishirikiana kushughulikia hali ya mambo katika eneo hilo. Lakini hii leo watu wa Sudan wamesahaulika.  

Vita kati ya mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al Burhan na makamu wake wa zamani, Mohamed Hamdan Daglo, ambaye anaongoza Kikosi cha wanamgambo kwa jina la Msaada wa Haraka (RSF) vimeua makumi ya maelfu, kuharibu miundombinu na kulemaza uchumi wa Sudan. 

Wababe wa vita Sudan, Dagalo (kushoto) na Al Burhan 

Katika vita vya sasa, Kikosi cha RSF na jeshi la Sudan vyote vinatuhumiwa kwa kushambulia maeneo ya makazi ya raia, kuwalenga raia na kuzuia usambazaji wa misaada ya kibinadamu. Shirika la WFP limesema kuwa kwa sasa haliwezi kufikia asilimia 90 ya wananchi wa Sudan wanaokabiliwa na tatizo la njaa; na kwamba ni asilimia tano tu ya watu wa Sudan ambao kwa siku wanaweza kumudu mlo kamili wa chakula.  

Tags