Afrika Kusini yatoa mwito wa kuwezeshwa wajasiriamali barani Afrika
(last modified Fri, 15 Mar 2024 02:48:30 GMT )
Mar 15, 2024 02:48 UTC
  • Afrika Kusini yatoa mwito wa kuwezeshwa wajasiriamali barani Afrika

Afrika Kusini imewataka viongozi na watunga sera wa nchi za Afrika kuandaa mazingira wezeshi kwa ajili ya wajasiriamali katika bara la Afrika ili kuhakikishwa wanapata ustawi na maendeleo yanayotakiwa.

Mwito huo umetolewa na Naibu Rais wa Afrika Kusini, Paul Mashatile, katika Kongamano la Kimataifa la Ujasiriamali Afrika (GEC+Africa) lililoanza Jumatano na kumalizika jana Alkhamisi mjini Cape Town.

GEC+Africa ni kongamano lililowakutanisha pamoja wajasiriamali na viongozi kutoka zaidi ya mataifa 50 ya Afrika na shabaha yake kuu ni kuendeleza shughuli za ujasiriamali katika nchi za bara hilo.

Kongamano hilo la siku mbili limehudhuriwa na zaidi ya wajumbe 1,500, wakiwemo wawakilishi wa biashara ndogo ndogo na za kati na kati (SMMEs), wawekezaji katika sekta mbalimbali, watunga sera na wawakilishi wa mashirika tofauti.

Vikao na mikutano ya kunyanyua hali ya wajasiriamali ni muhimu sana

 

Mashatile amesema: "Kongamano la GEC+Afrika limefanyika wakati mwafaka na muhimu sana kwa kuzingatia hali ya hivi sasa ya uchumi wa dunia hasa juhudi zinazoendelea barani Afrika za  kujipanga upya bara letu." 

Naibu huyo wa Rais wa Afrika Kusini amesema kuwa, bara la Afrika limefurika utajiri, suhula na uwezo wa kila namna ambao haujatumiwa hadi hivi sasa. Amesema Afrika ni kitovu cha uvumbuzi na ubunifu unaosubiri kuamshwa upya.

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Biashara Ndogondogo wa Afrika Kusini, Bi Stella Ndabeni-Abrahams ambaye naye amehutubia kongamano hilo ametoa mwito kwa serikali za Afrika kuunda mifumo wezeshi ili kusaidia ipasavyo ujasiriamali barani humo.

Amesema: "Mbali na kutunga sera, serikali lazima ziongoze na kutia nguvu mifumo yao ya kiikolojia ya ujasiriamali na ziweke mikakati imara ya kuisaidia sekta hiyo muhimu."