Mar 26, 2024 11:02 UTC
  • Malawi yatangaza janga la ukame huku El Nino ikileta njaa kusini mwa Afrika

Taifa la Malawi la kusini mwa Afrika limetangaza hali ya maafa kutokana na ukame katika wilaya 23 kati ya 28. Rais Lazarus Chakwera wa nchi hiyo inayopakana na Tazania amesema nchi yake inahitaji zaidi ya dola milioni 200 za msaada wa kibinadamu, chini ya mwezi mmoja baada ya nchi jirani ya Zambia pia kuomba msaada.

Rais wa Malawi amesema ametembelea maeneo mbali mbali ya nchi yake ili kubaini ukubwa wa janga la ukame, na tathmini ya awali ya serikali imegundua kuwa takriban asilimia 44 ya zao la mahindi la Malawi limepotoea, na kaya milioni 2 zimeathiriwa moja kwa moja. Amesema nchi hiyo yenye watu milioni 20 inahitaji karibu tani 600,000 za msaada wa chakula na kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kufikisha misaada haraka.

Malawi ni nchi ya hivi punde zaidi katika eneo hilo kutangaza uhaba mkubwa wa chakula kutokana na kiangazi kikubwa ambacho kimehusishwa na hali ya hewa ya El Nino.

Nchi ya tatu, Zimbabwe, pia imeshuhudia mazao yake mengi yakiharibika na watu nchini humo sasa wanakabiliwa na uhaba wa chakula. Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) mwishoni mwa mwaka jana lilitangaza kwamba mataifa mengi kusini mwa Afrika yalikuwa kwenye ukingo wa baa la njaa kwa sababu ya athari za El Nino.

WFP ilisema tayari kuna karibu watu milioni 50 kusini na sehemu za kati mwa Afrika wanaokabiliwa na uhaba wa chakula.

Mwezi uliopita ulikuwa wa kiangazi kikubwa katika kipindi cha miaka 40 kwa Zambia na Zimbabwe, huku Malawi, Msumbiji na sehemu za Angola zikiwa na "upungufu mkubwa wa mvua."