Mar 28, 2024 02:31 UTC
  • UNHCR yasema watu milioni 5.7 ni wakimbizi wa ndani DRC, yataka misaada

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi (UNHCR) limetoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka kutokana na ongezeko la hatari kwa watu waliokimbia makazi yao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Taarifa iliyotolewa na msemaji wa shirika hilo Matthew Saltmarsh mjini Geneva, Uswisi, imesema: “Miaka miwili ya mizozo katika maeneo ya Kivu Kaskazini huko Rutshuru na Masisi imewalazimisha zaidi ya watu milioni 1.3 kukimbia makazi yao ndani ya DRC, na kusababisha jumla ya watu milioni 5.7 kuwa wakimbizi wa ndani katika majimbo ya Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri.”

Ameongeza kuwa tangu mapigano makali yashike kasi katika mji wa Sake, tarehe 7 Februari, karibu watu 300,000 wamewasili katika jiji la Goma, ambako hali ilikuwa mbaya.

Watu zaidi ya 85,000 walikuwa wamekimbia ghasia hizo hizo na kutafuta makazi katika eneo la Minova la Kivu Kusini, ambalo tayari lilikuwa limepokea watu 156,000 waliokimbia makazi yao tangu Januari.

Ripoti hiyo pia imebaini kuwa mwaka jana 2023, shule 25 zilichukuliwa na vikundi vyenye silaha visivyo vya serikali katika maeneo ya Masisi na Rutshuru pekee, na shule zingine 17 zilishambuliwa.

Mwaka huu 2024, shule saba zimeharibiwa na milipuko ya mabomu.

Pia mwaka 2023, katika eneo la Kivu Kaskazini pekee, kulikuwa na kesi 50,159 zilizoripotiwa za unyanyasaji wa kijinsia, zaidi ya nusu ya kesi hizo zikiwa ni ubakaji, asilimia 90 ya waathirika hao walikuwa wanawake na wasichana, wakati asilimia 37 walikuwa ni watoto.

UNHCR inasema imepokea asilimia 14 tu ya dola milioni 250 zinazohitajika kwa ajili ya kukabiliana na hali ya wakimbizi na mahitaji yao nchini DRC kwa mwaka 2024.

Ukosefu wa fedha unatishia utoaji wa misaada, na hivyo kuzidisha janga baya la kibinadamu katika eneo hilo.