Apr 17, 2024 03:01 UTC
  • Nchi za Afrika zaendelea kupiga marufuku dawa ya kihokozi ya Marekani

Nchi kadhaa za bara Afrika zimepiga marufuku dawa ya kikohozi ya watoto iliyotengenezwa na kampuni ya Kimarekani ya Johnson & Johnson baada ya kubainika kuwa ina sumu inayoua watoto.

Katika hatua ya hivi karibuni, mamlaka husika za dawa  Tanzania, Rwanda na Zimbabwe zimeamuru kusitishwa matumizi ya dawa ya kikohozi kwa watoto ijulikanayo kama Benylin Paediatric Syrup iliyotengenezwa na kampuni ya Johnson & Johnson kama hatua ya tahadhari.

Hii ni baada ya mamlaka za Nigeria kusema kuwa vipimo vya maabara vilikuta viwango vikubwa vya sumu. Nchi hizo zinaungana na Nigeria, Kenya na Afrika Kusini katika kusitisha matumizi na kuamuru kurejeshwa dawa hiyo, ambayo inatumika kutibu kikohozi na homa kwa watoto.

Bodi ya Afya Nigeria imesema vipimo vya maabara kwenye dawa hiyo ya kikohozi vilionyesha kiwango kikubwa cha diethylene glycol, ambacho kimehusishwa na vifo vya makumi ya watoto nchini Gambia, Uzbekistan na Cameroon tangu 2022 katika moja ya mawimbi mabaya zaidi ya sumu duniani yaliyotokana na dawa za kumeza.

Msemaji wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba ya nchini Tanzania (TMDA) Gaudensia Simwanza amenukuliwa na vyombo vya habari vya kimataifa akisema kuwa mamlaka hiyo imeanza kuondoa dawa hizo kuanzia tarehe 12 Aprili, kufuatia taarifa za vipimo kutoka Nigeria."

Chanjo ya corona ya Johnson and Johnson ambayo pia iliripotiwa kusababisha vifo barani Afrika

Hili ni zoezi ambalo halihusishi uchunguzi bali ufuatiliaji ili kuhakikisha kuwa dawa zenye athari kwa matumizi ya binadamu zimeondolewa sokoni," Simwanza amesema.

Mdhibiti wa afya wa Nigeria alisema kuwa vipimo vya maabara vilivyo fanyika kwenye dawa hiyo vilionesha uwepo wa kiwango cha juu cha diethylene glycol, ambacho kimehusishwa na vifo vya makumi ya watoto nchini Gambia, Uzbekistan na Cameroon tangu 2022 katika moja ya milipuko mibaya zaidi ya sumu kusababishwa na dawa za kumeza duniani.

Dawa zilizorejeshwa zilitengenezwa na kampuni ya J&J nchini Afrika Kusini mwezi Mei mwaka 2021 kabla ya kuuzwa kwa kampuni ya Kenvue ambayo sasa inamiliki chapa ya Benylin Paediatric syrup.