Afrika Kusini yaiomba Mahakama ya ICJ: Israel 'lazima izuiwe'
(last modified Fri, 17 May 2024 08:22:35 GMT )
May 17, 2024 08:22 UTC
  • Afrika Kusini yaiomba Mahakama ya ICJ: Israel 'lazima izuiwe'

Afrika Kusini imeitaka Mahakama Kuu ya Umoja wa Mataifa iamuru kusitishwa uvamizi wa kijeshi dhidi ya Rafah kama sehemu ya kesi yake iliyofungua mjini The Hague inayoushutumu utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mauaji ya kimbari, ikisema utawala huo "lazima uzuiwe" ili kunusuru maisha ya Wapalestina.

Afrika Kusini iliwasilisha ombi hilo jana Alkhamisi katika siku ya kwanza kati ya mbili ya usikilizaji wa kesi hiyo katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ, inayojulikana pia kama Mahakama ya Dunia, baada ya hatua yake ya wiki iliyopita ya kuomba litolewe agizo la hatua za ziada za dharura kuulinda mji wa Rafah ulioko kusini mwa Ukanda wa Ghaza, ambao unatoa hifadhi kwa zaidi ya Wapalestina milioni moja.

Akizungumza mbele ya jopo la majaji wa ICJ, Mwanasheria wa Afrika Kusini Tembeka Ngcukaitobi amesema, mashambulizi ya kijeshi ya Israel yamelenga makumi ya maelfu ya watoto na wanawake, kuharibu miundombinu ya kiraia na kuiweka na njaa idadi kubwa ya watu.

Ameongezea kwa kusema: "tangu mwanzo dhamira ya Israel ilikuwa ni daima kuharibu maisha ya Wapalestina na kuwaondoa kwenye uso wa dunia. Rafah ndio hatua ya mwisho".

Adila Hassan, wakili mwingine anayewakilisha jopo la mawakili wa Afrika Kusini ameiambia jopo la majaji wa Mahakama ya ICJ: "Israel lazima izuiwe. Afrika Kusini iko mbele yenu tena leo kuiomba mahakama kwa heshima kutumia mamlaka yake...kuagiza marekebisho ambayo yataizuia Israel".

Afrika Kusini inaushutumu utawala wa Kizayuni kwa vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina. Mnamo Januari, Mahakama ya ICJ iliamuru Israel ihakikishwe wanajeshi wake hawafanyi mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina huko Ghaza, kuruhusu misaada zaidi ya kibinadamu na kuhifadhi ushahidi wowote wa ukiukaji wa hatua hizo, lakini utawala huo haujatekeleza agizo hata moja la mahakama hiyo…/