Msemaji: Mazungumzo ya kuondoa vikwazo dhidi ya Iran yanaendelea
(last modified Tue, 28 May 2024 02:48:35 GMT )
May 28, 2024 02:48 UTC
  • Msemaji: Mazungumzo ya kuondoa vikwazo dhidi ya Iran yanaendelea

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa mazungumzo ya kuondoa vikwazo dhidi ya Tehran yanaendelea.

Nasser Kanani alisema jana katika mkutano wa kila wiki na waandishi wa habari hapa Tehran kwamba, mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani kuhusu kuondoa vikwazo yanaendelea na akaongeza kusema: Timu ya mazungumzo ya Iran imekuwa ikifanya mazungumzo kwa kuwasiliana na taasisi za juu; na katika fremu hiyo imetumia suhula zote ndani ya serikali ili kufanikisha mazungumzo.   

Kuhusu uhusiano kati ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Kanani ameongeza kuwa  Iran ina mtazamo chanya kuhusu wakala wa IAEA na katika uwanja huo, inatarajiwa kwamba pande nyingine husika pia zitatilia maanani hatua athirifu za Iran na kujiepusha na uchukuaji hatua na maamuzi yanayokwamisha na kuvuruga mchakato wa kitaalamu na kiufundi wa Iran na wakala wa IAEA.  

Ushirikiano chanya kati ya Iran na IAEA 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran katika mkutano wake huo wa kila wiki na waandishi wa habari ameashiria pia hali ya mambo huko Ukanda wa Gaza na kusema jamii ya kimataifa ina wajibu na jukumu la kisheria na kimaadili kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na kwamba serikali ya Marekani ambayo ni muungaji mkono mkubwa wa utawala wa Kizayuni haijioni kuwa inabeba dhima na inapasa kuwajibika mbele ya maaamuzi yanayotolewa na taasisi muhimu za sheria za kimataifa.