Jun 18, 2024 07:08 UTC
  • Mashirika ya kiraia Senegal yataka kukatwa uhusiano wa nchi hiyo na Israel

Wanaharakati wa mashirika ya kiraia nchini Senegal wametoa mwito kwa serikali ya nchi yao kukakata uhusiano wa kidiplomasia na utawala haramu wa Israel, kutokana na jinai za kivita na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala huo wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Wanaharakati wa mashirika 19 ya kiraia katika nchi hiyo ya Afrika Maghairibi wameanzisha kampeni ya kuishinikiza serikali ya Dakar kuvunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Tel Aviv kutokana na mashambulizi ya umwagaji damu yanayofanywa na Wazayuni huko Gaza.

Mashirika hayo ya kulobi ambayo yaliitisha maandamano ya amani ya kuwatetea wananchi madhulumu wa Palestina mwezi uliopita, yanapanga kufanya maandamano mengine wiki ijayo, wakiwa na matumai kuwa serikali yao itakubali mwito huo. 

Haya yanajiri siku chache baada ya Waziri Mkuu wa Senegal kulaani jinai za Israel huko Gaza na kusisitiza kuwa, madola makubwa ya dunia yanayojigamba kulinda haki za binadamu yanahusika katika mauaji ya kimbari ya watu wa Palestina.

Osman Sonko alisema kuwa, wale wanaojinadi kuwa ni viranja wa demokrasia na watetezi wakubwa wa haki za binadamu duniani, leo hii ndio washiriki wakubwa wa mauaji ya halaiki ya watu wa Palestina.

Kadhalika Sonko alimwomba Rais wa Senegal kujiunga na kesi iliyofunguliwa na Afrika Kusini dhidi ya utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki ICJ.

Tags