Atiwa mbaroni baada ya kukiri kuua wanawake 42 Kenya
(last modified Mon, 15 Jul 2024 11:44:42 GMT )
Jul 15, 2024 11:44 UTC
  • Atiwa mbaroni baada ya kukiri kuua wanawake 42 Kenya

Polisi nchini Kenya imemkamata mshukiwa wa mauaji ya makumi ya wanawake viungani mwa mji mkuu, Nairobi.

Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) leo Jumatatu imetangaza kwamba mshukiwa huyo mkuu wa mauaji hayo katika eneo la Kware, mtaa wa Mukuru Kwa Njenga, viungani mwa Nairobi amekiri kuua zaidi ya wanawake 40.

DCI kwenye kikao na waandishi wa habari katika makao makuu yake jijini Nairobi, imemtaja mshukiwa huyo kuwa Collins Jumaisi Khalusa.

Mkurugenzi Mkuu wa DCI, Mohammed Amin ameeleza kwamba, Collins amekiri kuua wanawake 42 akiwemo mkewe, Imelda Judith, kati ya mwaka 2022 hadi Julai 11 mwaka huu, 2024,

“Mkewe alikuwa mwathiriwa wa kwanza, aligongwa (kwa kifaa butu) hadi akafa,” DCI Amin ameongeza. Mkuu huyo wa DCI amesema: “Mbinu iliyotumika ni moja. Miaka yao ni kati ya 18 hadi 30. Wote ni wanawake. Na miili hiyo imepakiwa na kufungwa kwa njia sawa.”

Collins alitiwa nguvuni usiku wa kuamkia leo Jumatatu katika mtaa wa Kayole jijini Nairobi, wakati akitazama finali za kipute cha Kandanda cha Bara Uropa (EURO 2024).

Amekamatwa baada ya kuopolewa kwa miili 13, kufikia jana Jumapili, kwenye timbo moja katika eneo la Kware jijini Nairobi. Awali ilidhaniwa kuwa, maiti hizo ni za vijana waliouawa wakati wa maandamano ya karibuni dhidi ya serikali.

Tags