Togo yateua tena mwanamke kuwa Waziri Mkuu kwa muda wa miaka sita
(last modified 2024-08-02T06:37:50+00:00 )
Aug 02, 2024 06:37 UTC
  • Togo yateua tena mwanamke kuwa Waziri Mkuu kwa muda wa miaka sita

Rais Faure Gnassingbe wa Togo jana Alkhamisi alimteua tena Victoire Tomegah-Dogbe kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo kwa muhula wa miaka sita chini ya katiba mpya.

Uteuzi huo umekuja miezi kadhaa baada ya Tomegah-Dogbe kujiuzulu wadhifa huo pamoja na serikali yake yote mwezi Machi mwaka huu.

Licha ya kujiuzulu, Gnassingbe alikuwa amempa Tomegah-Dogbe jukumu la kuendelea kusimamia masuala ya kusimamia mambo ya nchi hadi ilipoundwa timu mpya ya serikali.

Tomegah-Dogbe alikuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa waziri mkuu katika taifa hilo la Afrika Magharibi baada ya kuteuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2020.

Ameshikilia nyadhifa kadhaa za uwaziri tangu mwaka 2008, ikiwa ni pamoja na kuhudumu kama mkuu wa wafanyikazi wa ofisi ya rais.

Uteuzi wa jana Alkhamisi unafuatia kupitishwa katiba mpya na Bunge la Togo mapema mwaka huu, ambayo iliibadilisha nchi kutoka mfumo wa urais na kuwa mfumo wa bunge. Chini ya katiba mpya, rais atachaguliwa na bunge. 

Chini ya katiba mpya, mamlaka ya utendaji yapo kwa "mkuu wa baraza la mawaziri" yaani Waziri Mkuu.

Baba yake Rais Faure Gnassingbe yaani Gnassingbe Eyadema alitawala taifa hilo dogo la Afrika Magharibi kwa takriban miongo minne kabla ya mtoto huyo kutwaa madaraka kwa kuungwa mkono na jeshi.

Tags