Aug 04, 2024 02:33 UTC
  • UN yataka kuongezwa juhudi za kupeleka msaada wa haraka kwa waliokumbwa na njaa Sudan

Kaimu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya misaada amesema kuwa, janga la njaa katika jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan ni ukumbusho mzito wa wajibu wa jumuiya ya kimataifa kupeleka misaada ya kuokoa maisha mara moja.

Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Masuala ya Kibinadamu Joyce Msuya ambaye pia ni mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa amesema hayo na kuongeza kuwa, kuna udharura wa kuongeza juhudi za kuhakikisha kuwa misaada ya haraka inapelekwa magharibi mwa Sudan kuwasaidia watu waliokumbwa na njaa.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA), ambayo Msuya anaiongoza imesema kuwa, Awamu Jumuishi ya Usalama wa Chakula (IPC) iliripoti wiki hii kwamba, mgogoro wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan umeisukuma jamii ya watu wa Jimbo la Darfur Kaskazini katika janga la njaa, haswa katika kambi ya Zamzam karibu na makao makuu ya jimbo la El Fasher.

Amesisitiza kuwa: "Umoja wa Mataifa na washirika wake nchini Sudan wanafuatilia kwa karibu matokeo hayo ya janga hilo.

Amesema: "Watu wa Sudan wanaendelea kuteseka mno tangu mzozo ulipozuka zaidi ya miezi 15 iliyopita."

Amesema, njaa ni janga ambalo linaweza kutatuliwa ikiwa pande zote zitazingatia wajibu wao na ahadi zao kwa watu wwenye mahitaji makubwa.

Shirika la OCHA limesema kuwa, zaidi ya watu milioni 10 wamelazimika kuyahama makazi yao na kwamba zaidi ya nusu ya wakazi wa Sudan yaani watu milioni 25.6 wanakabiliwa na njaa kali.