Afisa wa jeshi la Libya aliyekuwa akisakwa na Interpol auawa mjini Tripoli
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115922-afisa_wa_jeshi_la_libya_aliyekuwa_akisakwa_na_interpol_auawa_mjini_tripoli
Watu waliokuwa na silaha wasiojulikana wamemuua kamanda wa kambi ya Chuo cha Jeshi la Wanamaji la Libya mjini Tripoli, Abd al-Rahman Milad, aliyepewa jina la utani la "Al-Bija," baada ya kummiminia risasi katika mjini Tripoli.
(last modified 2024-09-02T07:32:15+00:00 )
Sep 02, 2024 07:32 UTC
  • Afisa wa jeshi la Libya aliyekuwa akisakwa na Interpol auawa mjini Tripoli

Watu waliokuwa na silaha wasiojulikana wamemuua kamanda wa kambi ya Chuo cha Jeshi la Wanamaji la Libya mjini Tripoli, Abd al-Rahman Milad, aliyepewa jina la utani la "Al-Bija," baada ya kummiminia risasi katika mjini Tripoli.

Ripoti zinasema watu waliokuwa na silaha walilikamata gari la Meja Abd al-Rahman Milad katika mji wa Janzour (kitongoji cha magharibi mwa Tripoli) jana jioni na kumuua kwa kummiminia risasi.

Vyombo vya usalama tayari vimeanza uchunguzi wa tukio hilo.

Ingawa chanzo cha habari hii hakikuweka wazi utambulisho wa wauaji wa Bida au washukiwa wa mauaji hayo, lakini kimedokeza kuwa alikuwa na "maadui wengi." 

Chanzo hicho kimesema: "Tunatazamia kutokea machafuko katika mji mkuu kutokana na harakati za makundi yenye silaha yanayoshirikiana na Al Bija katika mji alikozaliwa wa Zawiya (kilomita 50 magharibi mwa Tripoli)."

Mkuu wa Baraza Kuu la la Utawala la Libya, Khaled Al-Meshri, ameomboleza kifo cha afisa huyo wa jeshi kwenye ukurasa wake rasmi wa Facebook.

Al-Meshri ametoa wito kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na mamlaka husika kuwafichua waliohusika na mauaji hayo na kuwafikisha mahakamani.

Al Bija anatajwa kuwa mmoja wa wafanya magendo ya binadamu wanaosakwa zaidi duniani, na aliwekewa vikwazo na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kuhusika moja kwa moja katika kuzama kwa boti za wahamiaji katika bahari ya Mediterania. 

Wahamiaji wakiwa Libya

Mnamo Juni 2018, "Al-Bija" alitajwa katika ripoti iliyotolewa na Baraza la Usalama kama "kiongozi wa genge hatari zaidi la magendo ya binadamu nchini Libya, linalohusika katika kuwatesa wahamiaji na kufanya ukiukaji wa haki za binadamu," huku Polisi wa Kimataifa (Interpol) wakitoa amri ya kukamatwa dhidi yake.