Misri yalalamika dhidi ya Ethiopia katika Umoja wa Mataifa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i115940-misri_yalalamika_dhidi_ya_ethiopia_katika_umoja_wa_mataifa
Misri imewasilisha malalamiko yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), ikiishutumu Ethiopia kwa kutishia uthabiti wa kikanda kwa hatua za upande mmoja kuhusu mradi wa kutatanisha wa Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (GERD) kwenye Mto Nile.
(last modified 2024-09-03T01:03:27+00:00 )
Sep 03, 2024 01:03 UTC
  • Misri yalalamika dhidi ya Ethiopia katika Umoja wa Mataifa

Misri imewasilisha malalamiko yake kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC), ikiishutumu Ethiopia kwa kutishia uthabiti wa kikanda kwa hatua za upande mmoja kuhusu mradi wa kutatanisha wa Bwawa la Grand Ethiopian Renaissance (GERD) kwenye Mto Nile.

Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya nje ya Misri, hatua hiyo imekuja kujibu kauli ya hivi majuzi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ambaye hivi karibuni alitangaza awamu ya tano ya kujaza bwara hilo bila kushauriana na mataifa yanayonufaika na Mto, haswa Misri.

Bwawa hilo liko kwenye Mto Blue Nile, ambao ni chanzo cha Aasilimia 97 ya maji ya Misri. Bwawa hilo ambalo limekuwa likijengwa tangu 2011, linatazamiwa kuwa mtambo mkubwa zaidi wa kuzalisha umeme barani Afrika mara tu litakapokamilika.

Malalamiko hayo ya Misri yanakuja wakati mvutano kati ya mataifa hayo mawili ya Kiafrika ukiongezeka kuhusu uungaji mkono wa Misri kwa Somalia, ambayo inakabiliwa na mzozo na Ethiopia kuhusu mpango wa kupata bandari.

Ethiopia ilitia saini makubaliano na eneo lilolojitenga la Somalia linalojulikana kama Somaliland mnamo Januari 1 kukodisha kilomita 20 (maili 12) ya ardhi ya pwani ili kujenga kambi ya jeshi la wanamaji. Somalia ililaani vikali mapatano hayo na kusema yanakiuka mamlaka yake ya kujitawala kwani haikuhusishwa.

Wiki iliyopita, Misri iliwasilisha msaada wa kijeshi, zikiwemo silaha, kwa Somalia kwa mara ya kwanza katika zaidi ya miongo minne, kufuatia makubaliano ya ulinzi yaliyotiwa saini mapema mwaka huu. Hatua hiyo ya Misri imepelekea Ethiopia kuingiwa na wasiwasi mkubwa kuwa ni sehemu ya mpango dhidi ya bwawa la GERD.