Umoja wa Mataifa warefusha vikwazo dhidi ya Sudan kwa mwaka mmoja mwingine
Sep 12, 2024 07:38 UTC
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limerefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Sudan kwa mwaka mmoja mwingine hadi Septemba 12, 2025.
Vikwazo hivyo vinajumuisha vile vinavyolenga watu maalumu pamoja na vikwazo vya silaha.
Rasimu ya azimio hilo iliyowasilishwa na Marekani, ilipitishwa kwa kauli moja na Baraza hilo lenye wanachama 15.
Azimio nambari 1591 la Umoja wa Mataifa lilipitishwa awali na Baraza la Usalama la umoja huo mnamo Machi 29, 2005, ili kuiwekea Sudan vikwazo kwa kulenga watu binafsi na vyombo vinavyohusika katika mzozo wa Darfur.
Linajumuisha marufuku ya kusafiri, kufungia mali na vikwazo vya silaha. Kamati ya vikwazo inayosimamia utekelezaji nayo pia ni sehemu ya azimio hilo pamoja na jopo la wataalamu wanaokusanya taarifa za utekelezaji wake na utoaji taarifa kwa Baraza.
Naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Robert Wood, amewashukuru wajumbe wa Baraza kwa ushirikiano wao wa kujenga upya utaratibu wa vikwazo dhidi ya Sudan kwa miezi 12 zaidi.../