Mali yaendelea 'kuviadhibu' vyombo vya habari vya Ufaransa
(last modified Thu, 12 Sep 2024 11:37:49 GMT )
Sep 12, 2024 11:37 UTC
  • Mali yaendelea 'kuviadhibu' vyombo vya habari vya Ufaransa

Serikali ya kijeshi ya Mali imepiga marufuku kanali nyingine ya televisheni ya Ufaransa kurusha matangazo yake kwa kukiuka Sheria ya Kudhibiti Vyombo vya Habari katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Mamlaka Kuu ya Mawasiliano ya Mali (HAC) imetangaza kuiondoa TV5 Monde ya Ufaransa kutoka kwenye orodha ya wasambazaji walioidhinishwa, kwa muda wa miezi mitatu.

HAC imesema uamuzi huo umechukuliwa kufuatia ukiukaji wa maandishi ya sheria na udhibiti ya Sheia ya Udhibiti wa Vyombo vya Habari, uliogunduliwa mnamo Agosti 26.

Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Agosti, serikali ya Mali ilipiga marufuku kanali ya televisheni ya Ufaransa ya LCI kurusha matangazo yake kwa muda wa miezi miwili kutokana na kile kilichotajwa kuwa upotoshaji kuhusu hali ya usalama wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi.

Vyombo vya habari vya Ufaransa vinatuhumiwa kwa upotoshaji na kukiuka sheria

Huko nyuma pia, Mali ilichukua hatua ya kusimamisha nchini humo matangazo ya Redio ya Kifaransa ya RFI na televisheni ya France 24 zinazofadhiliwa na serikali ya Ufaransa kwa muda wa miezi minne. Serikali ya kijeshi ya Mali wakati huo ilivituhumu vyombo hivyo vya habari kuwa vinaripoti habari za uwongo kwamba jeshi linaua raia.

Kadhalika serikali za Niger na Burkina Faso zimewahi kusimamisha nchini humo matangazo ya Redio ya Kifaransa ya RFI na televisheni ya France 24 zinazofadhiliwa na serikali ya Paris, kwa madai ya kutangaza habari za uwongo na upotoshaji.