Sep 14, 2024 04:28 UTC
  • Kaimu Mkuu wa Polisi nchini Kenya ahukumiwa kifungo cha miezi sita jela

Kaimu Mkuu wa Polisi nchini Kenya Ijumaa ya jana alihukumiwa kifungo cha miezi sita jela baada ya kukaidi mara kwa mara amri ya kutoa ushahidi kuhusu mahali walipo watu watatu ambao wametoweka baada ya kudaiwa kukamatwa na maafisa wa polisi.

Itakumbukwa kuwa watu hao watatu walikuwa wakijitokeza wazi wazi katika majukwaa ya kijamii kuunga mkono maandamano ya wananchi dhidi ya serikali mnamo Juni na Julai mwaka huu. 

Maandamano dhidi ya serikali 

Jaji wa Mahakama Kuu mjini Nairobi Lawrence Mugambi alikuwa ameakhirisha hukumu hiyo kwa siku saba ili kumpa Gilbert Masengeli, Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi nafasi ya mwisho kufika mahakamani kabla ya kuswekwa jela hata hivyo Masengeli hakuwahi kufanya hivyo.

"Ikitokea hatajisalimisha kwa Kamishna Jenerali (wa magereza), Waziri wa Mambo ya Ndani achukue hatua zote zinazostahili na zinazoruhusiwa kisheria kuhakikisha Gilbert Masengeli anafungwa jela,” Mugambi alisema katika agizo lake.

Wanaharakati wa haki za binadamu huko Kenya wanadai kuwa makumi ya watu walioshiriki katika maandamano dhidi ya serikali walitekwa nyara na makachero wa serikali ambapo aghalabu yao waliachiwa baadaye.

Rais William Ruto wa Kenya ameahidi kuchunguza tuhuma hizi tajwa ingawa ametetea pakubwa miendeno na utendaji wa idara za usalama wakati wa maandamano. 

 

Tags