Jeshi la Uganda: Tumefanikiwa kuwaondoa raia elfu 38 kutoka Sudan Kusini
(last modified Thu, 21 Jul 2016 04:32:41 GMT )
Jul 21, 2016 04:32 UTC
  • Jeshi la Uganda: Tumefanikiwa kuwaondoa raia elfu 38 kutoka Sudan Kusini

Jeshi la Uganda limetangaza kuwa, limefanikiwa kuwaondoa raia 38 elfu wa nchi kadhaa kutoka Sudan Kusini kutokana na machafuko yanayoendelea ndani ya nchi hiyo.

Taarifa iliyotolewa jana na jeshi hilo Uganda imesema kuwa jumla ya raia 39 elfu wa Uganda na mataifa mengine waliokuwa wamekwama mjini Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini, wamefanikiwa kuondolewa mjini hapo kupitia operesheni iliyoanza siku ya Ijumaa iliyopita. 

Askari wa Uganda wakielekea Sudan Kusini kuwaokoa raia

 

Paddy Ankunda, msemaji wa jeshi la Uganda amesema kuwa, raia hao waliokuwa Sudan Kusini wameondolewa na jeshi hilo kupitia njia ya barabara na chini ya ulinzi kamili wa jeshi la Uganda. Ameongeza kuwa, wengi wa walioondolewa nchini humo, ni Waganda na kwamba hata hivyo jeshi la Uganda liliwabeba raia wa Kenya, Rwanda na nchi nyingine kadhaa ambao walipendelea kuondoka Sudan Kusini. Operesheni za kuwaokoa raia wa Uganda waliokwama nchini Sudan Kusini zilianza siku ya Ijumaa kupitia njia ya barabara ambapo magari makubwa ya kijeshi yapatayo 30 ya jeshi la UPDF na jeshi la polisi yaliingia Sudan Kusini hadi mji mkuu wa nchi hiyo kwa minajili hiyo.

Tags