Makumi ya wanawake na watoto waokolewa kutoka mikononi mwa Boko Haram
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11764-makumi_ya_wanawake_na_watoto_waokolewa_kutoka_mikononi_mwa_boko_haram
Jeshi la Nigeria limewaokoa makumi ya wanawake na watoto kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi la Boko Haram.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 22, 2016 09:21 UTC
  • Makumi ya wanawake na watoto waokolewa kutoka mikononi mwa Boko Haram

Jeshi la Nigeria limewaokoa makumi ya wanawake na watoto kutoka mikononi mwa kundi la kigaidi la Boko Haram.

Kanali ya Televisheni ya France 24 imetangaza kuwa, jeshi la Nigeria limetangaza habari ya kuwaokoa takribani wanawake na watoto 80 waliokuwa wakishikiliwa mateka na kundi lenye misimamo mikali la Boko Haram. Kwa mujibu wa taarifa ya jeshi la Nigeria ni kuwa, wanawake na watoto hao wamekombolewa na jeshi hilo katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Bashasha na tabasamu baada ya kurejea nyumbani

Hivi karibuni pia jeshi la Nigeria lilitangaza kukombolewa wasichana kadhaa kutoka mikononi mwa wanamgambo wa Boko Haram ambao wametenda jinai kubwa nchini Nigeria na katika nchi za jirani.

Katika siku za hivi karibuni jeshi la Nigeria likishirikiana na lile la Cameroon limepata mafanikio ya kiwango fulani katika operesheni zao dhidi ya wanamgambo wa Boko Haram. Hata hivyo serikali ya Nigeria ingali inakosolewa kutokana na kushindwa kulitokomeza kundi hilo la kigaidi.

Baadhi ya wasichana na watoto waliookolewa na jeshi la Nigeria kutoka katika makucha ya Boko Haram

 

Hivi karibuni Benki ya Dunia ilitangaza kuwa, wanamgambo wa kundi la kigaidi la Boko Haram la nchini Nigeria hadi sasa wameua watu zaidi ya 20 elfu na kusababisha hasara ya dola bilioni 5.9 katika jimbo la Borno. Aidha ripoti hiyo ilisema zaidi ya watu milioni mbili wamefanywa wakimbizi kufuatia ugaidi wa kundi hilo la Boko Haram.