Mapigano makali yaibuka tena nchini Mali huku hali ya hatari ikitekelezwa
Mapigano makali yameibuka tena nchini Mali kati ya waasi wa Tuareg na makundi yanayoiunga mkobo serikali katika mji wa Kidali uliopo kaskazini mwa nchi hiyo ya Afrika magharibi.
Mapigano hayo mapya yanatokea siku moja tu baada ya kutangazwa hali ya hatari nchini humo. Mapigano hayo mapya yamewafanya raia katika mji wa Kidal kubakia majumbani mwao na kuogopa kutoka nje kutokana na kusikika milio ya risasi kila upande.
Watu wasiopungua 39 wakiwemo askari 17 wa jeshi la Mali waliuawa siku mbili zilizopita kufuatia shambulizi la umwagaji damu liliofanywa na waasi katika kituo kimoja cha kijeshi mjini Nampala katikati mwa nchi hiyo ya Magharibi mwa Afrika.
Kufuatia shambulio na mauaji hayo Rais Ibrahim Boubacar Keita alitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa huku akitangaza hali ya hatari kwa muda wa siku kumi.
Nchi ya Mali imekuwa ikikumbwa na mashambulizi ya makundi ya wabeba silaha katika maeneo ya kaskazini, tangu taifa hilo lilipokumbwa na mapigano ya mwaka 2012 na sasa maeneo ya katikati mwa nchi hiyo yamegeuka na kuwa uwanja wa machafuko.