UN: Vita vya Sudan vimesababisha watu milioni 14 kuwa wakimbizi
Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) limetangaza kuwa, vita vya zaidi ya mwaka mmoja na nusu huko Sudan vimepelekea watu zaidi ya milioni 14 kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.
Mkurugenzi Mkuu wa IOM, Amy Pope amewaambia waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi kwamba, watu zaidi ya milioni 14 wamekimbia nyumba zao kwa sababu ya vita vinavyoendelea huko Sudan tokea Aprili mwaka jana.
Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa ameeleza bayana kuwa, kuna haja kwa pande hasimu huko Sudan kusitisha mapigano.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji limesema kuwa, linahitaji msaada endelevu wa jamii ya kimataifa ili kutoa misaada na kuwalinda raia walioathiriwa na mapigano hayo.
Katika hatua nyingine, taarifa ya karibuni ya Shirika la Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) imesema: Kuna watoto milioni 3.7 walio na umri wa chini ya miaka 5 wanatarajiwa kukumbwa na utapiamlo mkali mwaka huu pekee na wanahitaji matibabu ya dharura ya kuokoa maisha yao.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, nusu ya wakazi wa Sudan yaani takriban watu milioni 25 wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi nchini humo.