Wahifadhi Qur'ani Tukufu nchini Nigeria waitaka serikali kuiunga mkono Palestina
Jukwaa la Huffadh wa Qur'ani Tukufu la Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria, limeandaa kongamano la siku mbili Jumamosi na Jumapili katika mji wa Potiskum wa Jimbo la Yobe Kaskazini Mashariki, ili kusisitiza uungaji mkono kwa mhimili wa muqawama ambao unapigana dhidi ya utawala katili wa Israel na pia kuwaombea dua mashahidi.
Katika kipindi cha Jumapili jioni, kipindi cha maswali na majibu kilifanyika kwa vijana wa kiume na wa kike waliohudhuria kozi ya kuhifadhi Qur'ani, ambapo hotuba ilitolewa na Sheikh Bala Afuwa kuhusu umuhimu wa kuunga mkono Mhimili wa Muqawama.
Wakati wa kikao cha usiku, usomaji wa Qur'ani Tukufu, dua ya ushindi kwa Mhimili wa muqawama na mihadhara ya Sheikh Abdullahi Hassan Azare ilifanyika.
Sheikh Bala Afuwa, ambaye alizungumza na Iran Press kwa niaba ya Jukwaa la Huffadh, ametoa wito kwa serikali ya Nigeria kufuata mfano wa Afrika Kusini na kuchukua hatua za kisheria za kuiwekea vikwazo utawala haramu wa Israel kwa jinai zake za kinyama dhidi ya binadamu huko Palestina na Lebanon.
Sheikh Bala Afwa amesema: "Kuna hatua kadhaa zinazopaswa kuchukuliwa na serikali ya Nigeria. Kwanza, tunaitaka serikali yetu kukata uhusiano wote wa kidiplomasia na utawala wa Israel, kisiasa na kiuchumi. Kiuchumi, tunaitaka serikali ya Nigeria kusitisha shughuli zote na Israel, na msaada wowote unaotolewa kwa Israel na serikali ya Nigeria unapaswa kukomeshwa haraka iwezekanavyo. Pili, kama raia tunaitaka serikali ya Nigeria kuchukua hatua kama ile iliyochukuliwa dhidi ya utawala wa Israeli na serikali ya Afrika Kusini. Ninachomaanisha ni kwamba Nigeria inapaswa kupeleka suala la Palestina katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) ili viongozi wa Israel waadhibiwe. Tatu, sisi Wanaigeria, tunataka serikali yetu iwaunge mkono Wapalestina, ukiwemo uungaji mkono wa kisiasa na kiuchumi. Hizi ni baadhi ya hatua tunazotaka serikali ya Nigeria izichukue dhidi ya utawala wa Kizayuni," amesema.