Sudan sasa yakumbwa na kipindupindu na homa ya kidingapopo
Nchini Sudan ambako vita na janga la njaa vinaendelea kuwahangaisha raia sasa wahudumu wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wanaonya juu ya tishio lingine kubwa la milipuko ya magonja ya kipindupindu na homa ya kidingapopo (dengue) huku mfumo mzima wa afya ukiwa taabani.
Kwa mujibu ya taarifa iliyotolewa Jumatatu mjini Geneva Uswisi na mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura OCHA na lile la afya duniani WHO, hali inazidi kuwa mbaya Sudan ambako katikati ya vita majanga mingine ya kiafya yanazuka.
OCHA imeripoti zaidi ya wagonjwa 28,000 wa kipindupindu na vifo vimefikia 836 katika majimbo 11 kati ya 22 Julai na 28 Oktoba mwaka huu huku likihofia kwamba idadi kamili ya wagonjwa huenda ni kubwa zaidi.
OCHA imeongeza kuwa mlipuko wa sasa wa kipindupindu umeshika kasi kufuatia msimu wa mvua kubwa isiyo ya kawaida ambayo ilisababisha mafuriko ambayo yalichafua vyanzo vya maji.
Kassala ndio jimbo lililoathiriwa zaidi likiwa na wagonjwa 6,868 na vifo 198, likifuatiwa na Gedaref, Al Jazirah, na jimbo la Kaskazini.
Wakati huo huo mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa yanasema ongezeko la homa ya kidingapopo nchini Sudan imekuwa kali pia haswa katika jimbo la Kassala na Khartoum.
Kufikia Oktoba 28, wagonjwa 4,544 wameripotiwa na vifo 12 vinavyohusiana na homa ya kidingapopo, huku Kassala pekee ikichukua zaidi ya nusu ya kesi hizi.
Hayo yanajiri huku Jeshi la Sudan likilendelea kukabiliana na waasi wa kundi la RSF ambao wameteka baadhi ya maeneo ya nchi hiyo na ambao wanatenda jinai za kivita ikiwa ni pamoja na kuharibu vituo vya matibabu.