Polisi Msumbiji yakamata kilo 573 za kokeini katika meli ya India
Polisi ya Msumbiji imekamata kilo 573 sawa na (pauni 1,263) za dawa za kulevya aina ya kokeini katika meli ya India. Haya yameelezwa na Idara ya Taifa ya Upelelezi ya nchi hiyo.
Hilario Lole, Msemaji wa Idara ya Taifa ya Upelelezi ya Msumbiji ameeleza kuwa dawa hizo za kulevya aina ya kokeini zimekutwa katika madumu ya lita 2,025 kwenye kontena lililobeba nyenzo za ujenzi.
Amesema, Idara ya Taifa ya Upelelezi ya Msumbiji imekamata dawa hizo za kulevya baada ya kupokea taarifa kuhusu kuwepo kwa bidhaa zenye kutia shaka katika moja ya makontena kadhaa ya meli moja ya India iliyotia nanga Msumbiji tarehe 3 mwezi huu wa Novemba.
Amesema baada ya kufanya uchunguzi wa kimaabara wa dawa hizo zilizokamatwa, walibaini kuwa ilikuwa mihadarati aina ya kokeini. Tayari Idara ya Taifa ya Msumbiji imeanzisha uchunguzi ili kuwatambua wamiliki wa dawa hizo za kulevya.
Msemaji wa Idara ya Taifa ya Upepelezi ya Msumbiji imesema, walanguzi wa kimataifa wa dawa za kulevya wameendelea kuitumia nchi hiyo kusafirisha dawa hizo kwenda sehemu mbalimbali duniani.
Kulingana na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali ya Msumbiji, zaidi ya tani 2.5 za kokeini, heroini na bangi zilinaswa nchini humo mwaka wa 2023.