Kanali Baratuza: Wanajeshi wa Burundi wataendelea kuhudumu katika kikosi cha AMISOM
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11965-kanali_baratuza_wanajeshi_wa_burundi_wataendelea_kuhudumu_katika_kikosi_cha_amisom
Msemaji wa jeshi la Burundi amesema kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo walioko nchini Somalia wataendelea kuhudumu chini ya mwavuli wa kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika (AMISOM).
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 25, 2016 09:43 UTC
  • Kanali Baratuza: Wanajeshi wa Burundi wataendelea kuhudumu katika kikosi cha AMISOM

Msemaji wa jeshi la Burundi amesema kuwa, wanajeshi wa nchi hiyo walioko nchini Somalia wataendelea kuhudumu chini ya mwavuli wa kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika (AMISOM).

Kanali Gaspard Baratuza amebainisha kwamba, kuanzia mwanzoni mwa mwezi huu hadi sasa takribani wanajeshi 2000 wa Burundi wametumwa nchini Somalia ili kuongeza nguvu katika kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika.

Amesema kuwa, wanajeshi wapya waliotumwa nchini humo wataendesha shughuli zao chini ya usimamizi wa Amisom lengo likiwa ni kuzipiga jeki operesheni za kijeshi za kikosi hicho zenye lengo la kulitokomeza kundi la wanamgambo wa al-Shabab. 

Wanajeshi wa Burundi wanaohudumu katika kikosi cha AMISOM Somalia

Burundi ni miongoni mwa nchi za Kiafrika zinazochangia kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika AMISOM nchini Somalia.

Baadhi ya wanajeshi wa AMISOM wakiwa kazini

Maafisa wa ngazi za juu katika jeshi la Burundi wameashiria vitisho vya wanamgambo wa kigaidi wa al-Shabab wa Somalia na kubainisha kwamba, kikosi cha AMISOM kimepata mafanikio ya kiwango fulani katika kurejesha amani na utulivu nchini humo.

Image Caption

Wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabab wamekuwa wakiwalenga askari wa serikali na wale wa kusimamia amani wa Umoja wa Afrika na kadhalika viongozi wa serikali wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Kundi hilo ambalo limeshatangaza utiifu wake kwa kundi la kigaidi la Daesh, linakusudia kuiondoa madarakani serikali ya Mogadishu na kuunda utawala wake.