Mauritania; mwenyeji wa mazungumzo ya amani ya Sudan
Mauritania Jumatano hii imekuwa mwenyeji wa mashauriano yenye lengo la kurejesha amani nchini Sudan kufuatia ombi la Umoja wa Mataifa na kwa ushiriki wa wajumbe kutoka nchi na mashirika mbalimbali.
Rais Mohamed Ould Ghazouni wa Mauritania amemlaki katika mji mkuu wa nchi hiyo, Nouakchott, Mjumbe wa Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ramtane Lamamra anayehusika na masuala ya Sudan. Mkutano huo wa leo umelenga kutafuta suluhu la mzozo wa Sudan, hasa katika maeneo yanayohusu masuala ya kibinadamu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Mauritania, Mohamed Salem Ould Merzoug, ameeleza kuwa mazungumzo hayo yamewakutanisha pamoja wadau katika jitihada za kusaka amani huko Sudan.
Sudan imetumbukia katika mapigano makali kati ya jeshi la nchi hiyo na Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) tangu mwezi Aprili mwaka jana. Pande mbili zinazozana kuhusu suala la marekebisho jeshini na kipindi cha mpito cha kisiasa.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa, mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan yamesababisha vifo vya watu zaidi ya elfu 20, mamilioni kuwa wakimbizi na kuwalazimisha wengine zaidi ya milioni 25 kuhitajia msaada mkubwa wa kibinadamu.