Uzalishaji mafuta wastawi Angola, mwaka mmoja baada ya kujitoa OPEC
Wastani wa uzalishaji wa mafuta kwa siku nchini Angola ulifikia mapipa milioni 1.134 katika robo tatu ya kwanza ya 2024, ikiwa ni ongezeko la asilimia 4 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana kabla ya kujitoa kwenye OPEC.
Hayo ni kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la Taifa la Petroli, Gesi na Nishati ya Mimea la Angola (ANPG).
Taarifa hiyo imesema kwamba, ongezeko hilo limeshuhudiwa baada ya Angola kujitoa katika Jumuiya ya Nchi Zinazouza Nje Mafuta kwa Wingi (OPEC) Disemba 21, 2023.
Angola ilijitoa kwenye jumuiya ya OPEC kutokana na kutoridhishwa na mgao wake wa uzalishaji wa mapipa milioni 1.11 kwa siku.
Takwimu za ANPG zinaonesha kuwa, mapato ya kila mwezi katika robo tatu za kwanza na mwezi Novemba kwa ujumla, yalipindukia kiwango cha awali kilichoidhinishwa na OPEC.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Angola, hatua za serikali ya nchi hiyo za kuleta utulivu zimechangia kuimarika uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu sana. Hata hivyo, pato limeendelea kwa kiasi kikubwa kuwa chini ya uzalishaji mkubwa wa mwaka 2015 ambapo wakati huo Angola ilikuwa inazalisha mapipa milioni 1.8 kwa siku.
Siku ya Ijumaa, Diamantino Pedro Azevedo, Waziri wa Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi wa Angola, alithibitisha dhamira ya serikali ya nchi hiyo ya kuendeleza uzalishaji wa mafuta wa zaidi ya mapipa milioni 1 kwa siku mwaka huu wa 2025, kwa lengo la kuistawisha sekta hiyo na kuhakikisha kunakuwa na utulivu wa usambazaji wa mafuta katika masoko ya ndani na nje ya nchi hiyo.