Sudan: Wanamgambo wa RSF wamekishambulia kituo cha umeme cha mji wa Dongola
(last modified Tue, 21 Jan 2025 07:11:53 GMT )
Jan 21, 2025 07:11 UTC
  • Sudan: Wanamgambo wa RSF wamekishambulia kituo cha umeme cha mji wa Dongola

Jeshi la Sudan limewatuhumu wanamgambo wa kikosi cha (RSF) kwa kukishambulia kituo cha umeme kaskazini mwa nchi hiyo na kusababisha kukatika kwa umeme katika mji wa Dongola.

Taarifa ya jeshi la Sudan imeeleza kuwa wanamgambo wa RSF wamekishambulia kituo cha umeme cha Dongola kwa kwa mashambulizi kadhaa ya droni. 

Shirika la Habari la Sudan (SUNA) limeripoti kuwa droni 10 zilikishambulia kituo hicho cha umeme na baadhi ya ndege hizo zisizo na rubani zilitunguliwa na mfumo wa ulinzi wa anga wa nchi hiyo. 

Shambulio hilo liliharibu moja ya transfoma ya kituo hicho na kusababisha kukatika kwa umeme katika jiji hilo. Hadi sasa kikosi cha RSF hakitoa taarifa yoyote ya kukanusha au kuthibitisha hujuma hiyo huko Dongola. 

Wanamgambo wa RSF 

Siku ya Jumamosi Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudan iliwatuhumu wanamgambo wa RSF kwa kushambulia vituo vya kuzalisha umeme na maji katika jimbo la al Qadarif mashariki mwa Sudan na kuwashambulia pia raia katika jimbo la al Jazirah. 

Mgogoro kati ya jeshi na RSF, unaoendelea tangu katikati ya Aprili 2023, umesababisha vifo vya watu zaidi ya 20,000 na wengine milioni 14 wamelazimika kuyahama makazi yao. Taarifa hii ni kwa mujibu wa takwimu za na Umoja wa Mataifa na mamlaka za serikali za mitaa za Sudan.