Mkuu wa IEBC aliyesimamia uchaguzi wa kwanza Kenya kubatilishwa na mahakama afariki
Wafula Wanyonyi Chebukati, aliyesimamia uchaguzi wa urais uliobatilishwa na Mahakama mwaka 2017 na 2022 ulioigawanya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ( IEBC) amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 63.
Chebukati, ambaye kitaaluma ni mwanasheria alichukua wadhifa wa uenyekiti wa IEBC mwaka 2017 uliokuwa ukitokota joto la kisiasa, wakati kiongozi wa upinzani Raila Odinga alipochuana na Rais Uhuru Kenyatta, ambaye alikuwa akigombea kwa muhula wa pili.
Mwenyekiti huyo wa IEBC wakati huo na timu yake walibebeshwa jukumu la kuendesha moja ya chaguzi zilizokuwa na ushindani mkubwa nchini Kenya ambao waliuandaa kwa muda wa chini ya miezi saba.
Hata hivyo, uchaguzi wake huo wa kwanza kusimamia ulipingwa, na matokeo ya kura za urais mwaka wa 2017 yakabatilishwa na Mahakama ya Juu katika uamuzi wa kihistoria.
Mahakama hiyo iliamuru uchaguzi mpya wa urais ufanyike ndani ya siku 60.
Hata hivyo, kiongozi wa upinzani Raila Odinga ambaye alishindwa, alisusia uchaguzi wa marudio, akisema hangeweza kushiriki uchaguzi uliosimamiwa na timu ile ile “iliyovuruga” ule wa awali.
Katika uchaguzi wa urais wa 2022 hali haikuwa tofauti, kwa sababu upinzani ulidai kuwa mgombeaji wake Raila Odinga, alitapeliwa na kwamba tume ilimpendelea mshindani wake William Ruto.
Hayati Chebukati aliyezaliwa Desemba 19, 1961, alikuwa na Shahada ya Kwanza ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, na Uzamili katika Utawala wa Biashara kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta.
Alikuwa mwanasiasa na mwanachama wa chama cha Orange Democratic Movement lakini alijiuzulu kabla ya kutuma maombi ya kuwa Mwenyekiti wa IEBC.../