Jul 31, 2016 16:18 UTC
  • 10 wauawa katika mashambulizi pacha ya mabomu Mogadishu

Kwa akali watu 10 wameuawa katika mashambulizi pacha ya mabomu ya kutegwa garini katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi mjini Mogadishu nchini Somalia.

Hussein Ali, ofisa mwandamizi wa polisi ya Somalia amesema, baada ya kujiri miripuko hiyo, wanamgambo hao walianza kufyatua risasi hovyo wakiwalenga maofisa usalama waliokuwa katika kituo hicho cha polisi. Walioshuhudia hujuma hiyo wanasema raia wanne waliokuwa nje ya makao makuu hayo ya Idara ya Ujasusi mjini Mogadishu ni miongoni mwa waliouawa.

Wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabaab la Somalia

Shambulio hilo limejiri masaa machache baada ya mji wa kiistratejia wa Garas-weyne uliokuwa chini ya udhibiti wa wanamgambo wa al-Shabaab kukombolewa na vikosi vya serikali vikishirikiana na Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM baada ya kujiri makabiliano makali kati ya pande mbili hizo.

Askari wa Kikosi cha Kusimamia Amani cha Umoja wa Afrika Somalia AMISOM wakishika doria

Juni 26, mashambulizi pacha ya mabomu yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 13 karibu na kambi ya AMISOM na nje ya ofisi za Umoja wa Mataifa katika mji mkuu Mogadishu.

Duru za polisi nchini humo ziliripoti kuwa, 7 miongoni mwa waliouawa katika hujuma hizo za kigaidi zilizofanyika karibu na uwanja wa kimataifa wa ndege mjini Mogadushu ni maafisa usalama.

Tags