Katumbi: Uchaguzi Kongo DR unapasa kufanyika kama ilivyopangwa
Kiongozi wa upinzani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambaye sasa yupo uhamisoni amesema uchaguzi wa Rais nchini humo ni lazima ufanyike katika muda ulioainishwa.
Moise Katumbi, kiongozi wa upinzani nchini Kongo aliyeko uhamishoni Ufaransa na ambaye anaonekana kuwa mpinzani mkuu wa Rais Joseph Kabila amesisitiza kuwa atashiriki katika uchaguzi wa rais wa mwaka huu wa Kongo na kutahadharisha kuwa uchaguzi huo unapasa kufanyika kama ilivyopangwa.
Kiongozi huyo wa upinzani nchini Kongo aliyeko uhamishoni ameyasema hayo huku Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo akipinga kurejea nchini kwa mpinzani wake huyo wa kisiasa. Muungano wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo mwezi Mei mwaka huu ulimuarifisha Moise Katumbi kuwa mgombea wake katika uchaguzi wa Rais wa mwaka huu.
Wakati huo huo juzi Jumatatu mzee Etienne Tshisekedi Mkuu wa Chama Kikuu kinachoipinga serikali alisisitiza mbela ya wafuasi wake kwamba Joseph Kabila hastahiki kugombea urais kwa mujibu wa katiba ya Kongo.