Wanahabari Nigeria wataka Israel iwekewe vikwazo vya mafuta, gesi
Mwenyekiti wa Muungano wa Waandishi wa Habari wa Nigeria (NUJ), Ibrahim Muhammad, ametoa wito kwa nchi za Kiislamu kuungana na kutumia nguvu zao za kiuchumi, hususan mafuta na gesi, kama nyenzo ya kukomesha mauaji ya kimbari ya Israel na Marekani huko Palestina na kwingineko.
Katika mahojiano na shirika la habari la Iran Press, Ibrahim Muhammad amelaani kimya cha jamii ya kimataifa na kuishutumu Israel na Marekani kwa kujaribu "kuufuta umma mzima wa Waislamu katika eneo la Mashariki ya Kati."
Ameonya kuwa, njama za Tel Aviv na Washington zinaenda mbali zaidi ya Palestina na zinataka kutawala eneo zima. "Madhali mataifa ya Kiislamu yamefarakanishwa, hayawezi kukomesha uovu huu," ameongeza.
Mwenyekiti huyo wa Muungano wa Waandishi wa Habari wa Nigeria amebainisha kuwa, "Mafuta ni silaha yenye nguvu. Ikiwa nchi za Kiislamu zitaacha kuziuzia mafuta Israel, Marekani, na washirika wao, mauaji ya kimbari yatakoma. Lakini lazima wachukue hatua kwa pamoja na sasa hivi."
Licha ya kulaaniwa kimataifa, lakini Israel inaendelea na mashambulizi yake ya kikatili huko Gaza kwa msaada kamili wa Marekani, sanjari na kuzuia chakula na misaada ya kibinadamu, kuwalenga raia, na kukiuka sheria na kanuni za kimataifa.
Mgogoro wa kibinadamu unazidi kuongezeka katika Ukanda wa Gaza, huku taasisi za kimataifa zikishindwa kukomesha umwagaji damu na jinai wanazofanyiwa Wapalestina na Wazayuni.