Kushadidi mivutano ya kisiasa nchini Tunisia
Sambamba na bunge la Tunisia kukataa kumpa ridhaa Waziri Mkuu Habib Essid ya kuendelea kushika wadhifa huo mivutano ya kisiasa imeshtadi nchini humo.
Baadhi ya viongozi wa vyama vinavyounda serikali ya mseto ya Tunisia vilimtaka Essid ajiuzulu wadhifa wake ili kutoa fursa ya kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa. Zaidi ya hayo hitilafu kubwa zilizokuwepo baina ya Rais Beji Caid Essebsi na Habib Essid zilitatiza utendaji wa serikali ya Essid.
Hatimaye bunge likaachiwa mamlaka ya kuamua kama Waziri Mkuu Habib Essid aendelee kuhudumu katika wadhifa wake huo au la. Wabunge 118 waliunga mkono hoja ya kutokuwa na imani na serikali ya Waziri Mkuu Habib Essid ambaye alikuwa ameshikilia wadhifa huo kwa muda wa mwaka mmoja na nusu. Ni wabunge watatu tu waliunga mkono serikali ya Essid na waliosalia waliamua kutopiga kura.
Serikali ya Habib Essid iliingia madarakani mwezi Februari mwaka uliopita wa 2015 na mnamo Januari 2 mwaka huu ilifanya mabadiliko makubwa katika safu ya mawaziri; hata hivyo lawama na ukosoaji kuhusu kushindwa kuboresha uchumi na kupambana na ufisadi uliendelea kuiandamana serikali hiyo siku baada ya siku.
Katika hotuba aliyotoa kama jibu na radiamali yake kwa uamuzi wa bunge kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye Essid aliashiria uchaguzi ujao wa bunge na kueleza kwamba mabadiliko na upanguaji wowote utakaofanywa serikalini utakuwa na matokeo hasi kwa hali ya ndani ya Tunisia. Akaongezea kwa kusema, kazi ya kupambana na ugaidi ni nyepesi zaidi mara kadhaa kulinganisha na kupambana na ufisadi katika nchi hiyo. Katika hali na mazingira hayo, ofisi ya Rais Essebsi imetoa taarifa na kueleza kwamba imesainiwa hati maalumu ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa kwa madhumuni ya kuitoa nchi kwenye kinamasi cha mgogoro ambao ulikuwa umeitanza serikali mpya ya miezi sita ya Habib Essid. Hati hiyo iliyopewa jina la "Makubaliano ya Carthage" imesainiwa na vyama tisa vikubwa vikiwemo vinne vinavyounda serikali ya mseto ya sasa, yaani Nidaa Touneskilichoshinda uchaguzi wa bunge was mwaka 2014, chama cha harakati ya Kiislamu ya An-Nahdhah kilichoshika nafasi ya pili kwenye uchaguzi huo, Free Patriotic Union na Afek Tounes.
Sambamba na hayo baadhi ya vyombo vya habari vimeripoti kuwa Habib Essid amefanywa mbuzi wa kafara la kisiasa. Tovuti ya habari ya Public Finance International ilichapisha ripoti hapo jana na kueleza kwamba Habib Essid hakuweza kuupatia tiba uchumi wa Tunisia kwa kutegemea dawa ya sera za kiuchumi za Kimarekani. Hata hivyo mtazamo huo umepingwa na Katibu Mkuu mpya wa chama cha An-Nahdhah Ziyad al-A'dhari.
Al-A'dhari amesisitiza kuwa hatua iliyochukuliwa haijamlenga Waziri Mkuu au mtu mwengine yeyote yule, bali lengo lake ni kuharakisha utekelezaji wa mpango wa kurejesha tumaini na matarajio kwa wananchi wa Tunisia. Katibu Mkuu huyo wa chama cha An-Nahdhah aidha amesema serikali itakayoundwa kwa lengo hilo itaelekeza nguvu zake katika kupambana na ufisadi na kuandaa mkakati wa kitaifa utakaokubaliwa na vyama muhimu vya siasa, vya kijamii na ya kiraia vya nchi hiyo.
Hivi sasa tetesi zinazidi kuongezeka katika anga ya kisiasa ya Tunisia kuhusu uteuzi wa mtu atayerithi nafasi iliyoachwa na Habib Essid huku baadhi ya duru zikiripoti kuwa Rais Beji Caid Essebsi amependekeza jina la Waziri wa Masuala ya Ndani Yusuf Shahid, ambaye ni mkwe wa kiongozi huyo, kushika wadhifa huo.../