Mhadhiri Ghana: Kimya cha dunia kwa jinai za Israel Gaza kinaaibisha
Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Ghana,Mustapha Abdullah Kuyateh amelaani vikali hujuma za kikatili za Israel dhidi ya Gaza, akisisitiza kuwa huo ni mwendelezo wa mauaji ya kimbari na mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina.
Katika mahojiano maalum na Iran Press, Kuyateh huku akiashiria maelfu ya vifo na uharibifu mkubwa uliosababishwa na operesheni zinazoendelea za kijeshi za Israel, ameushutumu utawala wa Kizayuni kwa kufanya jinai dhidi ya binadamu.
Huku akisisitiza kuwa mauaji ya Gaza ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa za kibinadamu, Kuyateh amesema jinai hizo za Wazayuni katika zinatia aibu, na ni doa kwa jamii ya mwanadamu.
Ameilaumu jamii ya kimataifa, hasa Umoja wa Mataifa, Baraza la Usalama la umoja huo, na Marekani, kwa kimya chao na kushindwa kuchukua hatua za kuzuia mauaji hayo ya kimbari Gaza.
Msomi huyo wa Ghana ametoa wito kwa dunia kuchukua hatua za kuuwajibisha utawala wa Kizayuni, akisisitiza kuwa kimya cha taasisi za kimataifa kinafedhehesha.

Kuyateh ameeleza bayana kuwa, ari na moyo wa mapambano ya Wapalestina kamwe haitazimwa na kwamba, Wapalestina wataendelea kusimama kidete kupigania haki zao.
Mhadhiri huyo mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Ghana ameeleza kuwa, kutochukuliwa hatua na kutobebeshwa dhima kumeiwezesha Israel kuendelea na operesheni zake za kijeshi bila woga wala kizuizi.