UN: Mauaji ya mamia ya watu El-Fasher, Sudan yanatisha
(last modified Tue, 15 Apr 2025 07:59:47 GMT )
Apr 15, 2025 07:59 UTC
  • UN: Mauaji ya mamia ya watu El-Fasher, Sudan yanatisha

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amelaani vikali mashambulizi mabaya ya hivi karibuni ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) huko eneo la Darfur Kaskazini nchini Sudan akisema kuwa, mashambulizi hayo yanaashiria kushindwa kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua za maana licha ya maonyo ya mara kwa mara.

Volker Turk alisema hayo katika taarifa yake ya jana Jumatatu na kueleza kuwa: Mashambulizi makubwa kwenye kambi za wakimbizi wa ndani za Zamzam na Abu Shouk mji wa El Fasher, na eneo la Um Kadada yameua mamia ya raia, wakiwemo wafanyakazi wa asasi za misaada ya kibinadamu wasiopungua tisa.

"Mashambulizi haya yameweka wazi matokeo ya kutochukua hatua kwa jumuiya ya kimataifa, licha ya onyo langu la mara kwa mara la hatari kubwa kwa raia katika eneo hilo - ikiwa ni pamoja na onyo la Ijumaa iliyopita," Turk amesema.

Amesema vurugu hizo zimezidisha hali ambayo tayari ni janga huko El Fasher, ambayo imestahimili kuzingirwa kwa muda mrefu kwa RSF tangu Mei 2023. Pia alielezea wasiwasi wake juu ya hatari inayoongezeka ya dhulma za kikabila dhidi ya raia wanaodhaniwa kuwa na mfungamano na Wanajeshi wa Sudan (SAF).

Kabla ya hapo, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Mahmoud Ali Youssouf alielezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka ghasia nchini Sudan, hasa katika eneo la Darfur Kaskazini. Youssouf ameelezea kusikitishwa na hali ilivyo hivi sasa wakati alipokuwa anatoa ripoti za mashambulizi makali karibu na El Fasher ikiwa ni pamoja na mashambulizi mabaya katika kambi za wakimbizi za Zamzam na Abu Shouk.

Wapiganaji wa RSF

Harakati ya Jeshi la Ukombozi wa Sudan, inayoongozwa na Minni Arko Minnawi (SLA-Minnawi), gavana wa jimbo la Darfur magharibi mwa nchi hiyo, imetangaza kuwa watu 450 wameuawa kutokana na mashambulizi ya siku ya tatu mtawalia yaliyofanywa na wapiganaji wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF) katika mji wa El Fasher, makao makuu ya eneo hilo, na kwenye kambi za wakimbizi.

Tangu Aprili 15, 2023, RSF imekuwa ikipambana na jeshi la Sudan kwa ajili ya kudhibiti nchi, na kusababisha maelfu ya vifo na mojawapo ya migogoro mbaya zaidi ya kibinadamu duniani.