Maandamano ya wananchi Morocco; nara dhidi ya jinai za Israel
(last modified Tue, 22 Apr 2025 13:11:47 GMT )
Apr 22, 2025 13:11 UTC
  • Maandamano ya wananchi Morocco; nara dhidi ya jinai za Israel

Wananchi wa Morocco wameandamana kuunga mkono Wapalestina wanaoishi katika Ukanda wa Gaza na kupinga meli zinazobeba zana za kijeshi za utawala wa Kizayuni kutia nanga katika bandari za nchi yao.

Washiriki wa maandamano hayo pia wamesisitiza uungaji mkono wao kwa malengo mtaukufu ya Wapalestina na kupinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Ripoti zinasema, washiriki wa maandamano hayo makubwa walipiga nara dhidi ya kutia nanga meli zinazoelekea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, kulaani jinai za jeshi linalokalia kwa mabavu katika Ukanda wa Gaza, mauaji ya halaiki ya Wapalestina wanaoishi katika Ukanda wa Gaza, pamoja na kuwatimua Wapalestina kwa lazima, na kuwalenga kwa mashambulio wafanyakazi wa sekta ya misaada.

Miongoni mwa nara zilizotolewa na wananchi wa Morocco katika maandamano hayo ni: "Watu wa Morocco wanapinga kuanzishwa uhusiano wa kawaida na Israel," "Tuko tayari kufa kwa ajili ya Gaza," "Wameiuza Gaza kwa sarafu ya dola," na " ni fedheha kutia nanga meli katika bandari ya Casablanca."

Washiriki wa maandamano hayo aidha wameeleza kuchukizwa kwao kuwa pamoja Marekani na nchi za Magharibi na Israel na misimamo ya kufedhehesha ya ulimwengu wa Kiarabu kuhusiana na suala hilo, na kutoa wito wa kukomeshwa mauaji ya Wapalestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni kama ambavyo wameitaka serikali ya Morocco kufuta makubaliano yake ya kuanzisha uhusiano na Tel Aviv.

Katika siku za hivi karibuni, meli kutoka kampuni ya meli ya Denmark ya Maersk ilitia nanga katika bandari ya Maghreb. Maersk ni mojawapo ya mashirika makubwa  zaidi ya meli duniani na imekuwa ikifanya kazi kwenye uga wa kijeshi na kiraia kwa miaka mingi. Historia ya kampuni hiyo ya kusafirisha shehena za kijeshi kwa ajili ya NATO, Marekani na washirika wake imesababisha baadhi ya mashirika ya kiraia ya Morocco kutaka kuwekwa wazi kuhusu asili ya mizigo hiyo inayopitia bandari za nchi yao.

 

Kampuni hiyo inatuhumiwa kusafirisha zana na silaha za kijeshi za Marekani  na kuupelekea utawala wa Israel kwa ajili ya matumizi katika vita vya Gaza, na njia yake ya baharini inapitia baadhi ya bandari za Morocco, ikiwemo ya Casablanca.

Kwa mujibu wa habari zilizopatikana, shehena hizi hupakiwa kutoka katika vituo vya Marekani vilivyoko Ulaya au Marekani na kuelekea kwenye bandari za Israel katika Bahari ya Mediterania, kwa kutumia bandari za Morocco kama vituo vya kujaza mafuta na kupakia tena njiani, kitendo ambacho wanaharakati wengi wa kisiasa na haki za binadamu wanaona kuwa ni aina ya ushiriki usio wa moja kwa moja katika vita dhidi ya Wapalestina.

Makubaliano ya kuweko uhusiano wa kawaida kati ya Morocco na utawala wa Kizayuni yalifikiwa mwezi Disemba 2020. Marekani iliiahidi Morocco kuwa italitambua eneo la Sahara Magharibi kuwa ni milki ya Morocco kwa sharti kwamba utawala wa kifalme wa nchi hiyo uwe na uhusiano wa kawaida na utawala katili wa Kizayuni. Uamuzi huo wa kisiasa wa serikali ya Morocco ulikuwa unasubiri kisingizio tu kwa sababu viongozi wa nchi hiyo walikuwa muda mrefu wanajaribu kuunganisha msimamo wao wa kidiplomasia na kikanda kupitia makubaliano kama hayo ili wapate msaada wa kiuchumi na kijeshi wa Marekani.

Tangu kutiwa saini mkataba huu, wananchi wa Morocco ambao wana mizizi mirefu ya Kiislamu na Kiarabu na wamejikita kwenye kuliunga mkono taifa la Palestina, wameonesha mara kwa mara upinzani wao dhidi ya maamuzi ya watawala wa nchi hiyo kupitia kufanya mikutano mikubwa huko Rabat na kwenye miji mingine.

Maandamano hayo yameshika kasi katika miaka michache iliyopita hususan tangu kuanza Vita vya Gaza na jinai kubwa zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, wananchi wa Morocco mbali na kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina, mara kadhaa wametoa mwito wa kufutwa makubaliano ya kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni.

Mohammed Al-Riahi Al-Idrisi, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Morocco, anasema kuhusiana na suala hili: "Watu wa Morocco wanapinga bandari zetu kuhudumia meli zinazoelekea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu; hii ni pamoja na ukweli kwamba, Gaza iko chini ya mzingiro mkali na mauaji na Wapalestina hawaruhusiwi kupokea hata mahitaji rahisi na ya awali kabisa. Aidha anasisitiza kuwa,  kuanzisha uhusiano wa kawaida na wauaji na watenda jinai, ni jinai mbaya na ushiriki halisi katika kumwaga damu za watu wa Palestina."

 

Tangu kuanza kwa vita vya Gaza, zaidi ya Wapalestina 51,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa shahidi, na miundombinu yote, nyumba na maeneo huko Gaza yameharibiwa. Hata katika kipindi kipya baada ya usitishaji mapigano kuvunjwa, mahema ya Wapalestina wanaoishi Gaza yanachomwa moto. Aidha, kizuizi kamili cha chakula na dawa kinaendelea. Sasa Gaza imegeuzwa kuwa eneo la majanga na maafa.

Katika hali hii, kuwasili kwa meli za Maersk katika bandari za Morocco kumesababisha mlipuko wa hasira ya umma. Ukweli ni kuwa, Wamorocco wengi wanapinga nchi yao kuwa na uhusiano wa kawaida na  Israel. Wanalichukulia suala la Palestina kama sehemu ya utambulisho wao wa Kiislamu na Kiarabu na wanaamini kwamba, Tel Aviv ni nembo ya uvamizi, mauaji ya halaiki na ukoloni mamboleo katika eneo hilo. Hata hivyo, serikali ya Morocco imeendelea kudumisha uhusiano na Israel, ikipuuza matakwa ya watu.

Katika mazingira haya, vuguvugu la maandamano huko Casablanca na miji mingine ya Morocco sio tu ni jibu la kuwepo kwa meli bandarini, bali ni sauti ya kuwa pamoja na machungu ya ukandamizaji wa watu wa Palestina. Huku waandamanaji wa Morocco, wakiwa na bendera za Palestina, picha za watoto wahanga huko Gaza, na mabango ya kupinga "kuwa na uhusiano wa kawaida na Israel" na "ukaliaji mabavu," walitoa mwito wa kusitishwa ushirikiano wowote na Israel. Moja ya kauli mbiu kuu za waandamanaji ni: "Casablanca ni bandari ya muqawama, si njia na kivuko  cha wauaji wa watoto wa Gaza."

Inaonekana kuwa, maandamano ya hivi karibuni yanaweza kuwa mwanzo wa wimbi jipya la upinzani wa wananchi wa Morocco kwa mchakato wa kuanzisha uhusiano wa kwaida na Israel.