Wamorocco wavunja "daraja" lililobeba zawadi angamizi za Marekani
Wafanyakazi nchini Morocco wamekuwa ngome ya kuwalinda watoto wa Ghaza baada ya kukataa kupeleka zawadi angamizi za Marekani kwa utawala dhalimu wa Israel.
Hayo yameripotiwa na gazeti la Morocco la "Hespress" ambalo limeongeza kwamba, wafanyakazi kadhaa wa kampuni moja ya Denmark wamestahabu kujiuzulu kazi zao katika bandari ya Tangier nchini Morocco ili kukwepa wasitumike kupeleka silaha za Marekani kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Wafanyikazi hao wa kampuni moja ya Denmark wamesema kuwa meli ya Marekani iliyobeba silaha zinazopelekwa kwa Israel hadi hivi sasa imetia nanga katika bandari ya Tangier kaskazini mwa Morocco kwani wafanyakazi wamegoma kutumia nguvu zao kusaidia kupelekewa Israel silaha hizo angamizi zinazotumika kuua wanawake na watoto huko Ghaza.
Duru za habari za Morocco zimetangaza kuwa, silaha hizo zilipangiwa kufikishwa kwenye ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni ndani ya siku chache zijazo lakini mchakato wa kupelekwa silaha hizo umeingia dosari kutokana na kugoma wafanyakazi wa Kampuni ya Maersk ya Denmark ambayo ndiyo iliyobeba jukumu la kupeleka kidogokidogo silaha hizo za Marekani hadi kwenye bandari ya Haifa ili zitumike kuulia watoto wadogo wa Palestina. Gazeti la Hespress limeongeza kuwa kampuni ya Maersk ya Denmark iliwalazimisha wafanyakazi wake kushusha shehena hiyo, lakini wengi walikataa na kulizuka fujo. Baadhi ya wafanyakazi hao wameamua kujiuzulu ili wasishiriki kwenye jinai za Israel.
Ingawa baadhi ya nchi za Kiarabu zimetangaza kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala katili ya Kizayuni, lakini wananchi wa nchi hizo hawako pamoja na tawala zao.