Makumi ya familia za Warundi zarejea nyumbani
Gavana wa mkoa mmoja kaskazini mashariki mwa Burundi ametangaza habari ya kurejea mamia ya familia za raia wa Burundi waliokuwa wamekimbilia nchini Tanzania.
NJiji Desire, Gavana wa mkoa wa Cankuzo unaopatikana kaskazini mashariki mwa Burundi amesema kuwa familia 70 zilizokuwa zikiishi kama wakimbizi katika kambi ya Nduta nchini Tanzania tayari zimewasilia katika eneo la Mishiha katika mkoa wa Cankuzo. Ripoti kutoka Tanzania zinasema kuwa familia 70 kati ya 175 za Warundi ambazo zilikuwa zikiishi katika kambi ya wakimbizi ya Nduta zimerejea Burundi. Wakati huo huo viongozi wa serikali ya Burundi wamekaribisha kuendelea kurudi nyumbani raia wengi wa nchi hiyo. Shirika la Msalaba Mwekundu limeanzisha huduma za mawasiliano katika kambi mbalimbali za wakimbizi nchini Tanzania ili kurahisisha mawasiliano kwa wakimbizi hao wa Burundi. Njia hiyo ya mawasiliano imeandaa uwanja wa kurudi nyumbani raia wa Burundi waliokimbilia Tanzania kufuatia machafuko ya kisiasa yaliyoikumba nchi yao. Ni zaidi ya mwaka mmoja sasa ambapo Burundi imetumbukia katika machafuko ya kisiasa yaliyosababisha mapigano ya umwagaji damu, kufuatia hatua ya Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kutangaza azma yake ya kugombea kiti cha urais kwa muhula mwingine wa tatu; kitendo ambacho wapinzani wake wanadai ni kinyume na katiba ya nchi.