Umoja wa Mataifa wapunguza msaada wa kibinadamu DRC
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, umepunguza kwa karibu nusu malengo yake ya misaada ya kibinadamu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Taarifa ya Umoja wa Mataifa imesema, matatizo ya ufadhili yanaulazimisha kuzingatia tu watu wenye uhitaji mkubwa zaidi.
Mwezi Februari mwaka huu, Umoja wa Mataifa ulitoa ombi la karibu dola bilioni 2.5 kuwasaidia watu milioni 11 katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwaka huu badala ya milioni 21 ambao Umoja wa Mataifa unawaona kuwa wanahitaji msaada.
Ofisi ya masuala ya kibinaadamu OCHA imesema imeweka vipaumbele vipya kwa sababu msaada unapungua na mahitaji yanaongezeka. OCHA imesema kwa kuwa ni msaada wa dola milioni 245 pekee ambao umepokelewa kujibu ombi hilo hadi sasa, mpango huo mpya umebainisha "hatua za kuokoa maisha zitakazowasaidia watu milioni 6.8 walio hatarini zaidi kwa gharama ya dola bilioni 1.25 takriban nusu ya mahitaji ya mpango kamili."
Hatua hiyo ya kupunguzwa kwa misaada inajiri wakati mashirika mengi ya Umoja wa Mataifa yakipunguza operesheni zao na idadi ya wafanyakazi kote ulimwenguni huku wafadhili wakipunguza bajeti.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, hali mbaya ya kibinadamu inaripotiwa katika baadhi ya maeneo ya Jamhuri ya Kiemokrasia ya Congo kutokana na kuendelea ghasia na machafuko.
Kundi la M23, lililo katikati ya mzozo wa mashariki mwa Kongo, limeongeza mashambulizi yake tangu Desemba, likiteka miji muhimu ikiwemo Goma na Bukavu. Kinshasa na wengine wanailaumu Rwanda jirani kwa kuwaunga mkono M23 — madai ambayo Kigali inakanusha.