Jeshi la Sudan latwaa tena eneo la kimkakati Darfur Kaskazini kutoka kwa RSF
Jeshi la Sudan limefanikiwa kutwaa tena udhibiti wa eneo muhimu la kistratajia la Attrun huko Darfur Kaskazini kutoka kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).
"Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan na Vikosi vya Pamoja vimepata ushindi mkubwa kwa kukomboa eneo la kimkakati la Attrun kutoka mikononi mwa wanamgambo wa kigaidi wa RSF," Gavana wa Darfur, Minni Arko Minnawi amesema katika ujumbe wake aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Facebook.
Vikosi vya Pamoja vilitoa taarifa kuthibitisha kuwa eneo la Attrun sasa liko chini ya udhibiti wa jeshi. Ilisema kikundi cha wanamgambo kilipata "hasara kubwa ya maisha na vifaa." Hakuna taarifa iliyotolewa na RSF kufikia sasa juu ya tukio hilo.
Wakati huo huo, raia wasiopungua 14 waliuawa jana Jumapili wakati wapiganaji wa RSF walipoanzisha mashambulizi ya mizinga huko El Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini magharibi mwa Sudan.
"Raia kumi na wanne waliuawa leo (jana) kutokana na kushambuliwa kwa mizinga na wanamgambo wa RSF," Kamati ya Uratibu wa Upinzani huko El Fasher imesema katika taarifa.
Ilibainisha kuwa, mashambulizi hayo yalilenga Soko la Naivasha katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Abu Shouk, pamoja na vitongoji kadhaa kaskazini mwa El Fasher.
Jeshi la Sudan limekuwa likipambana na waasi wa RSF tangu Aprili 2023, na vita hivyo vimepelekea vifo vya maelfu ya watu na kusukuma Sudan katika moja ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani.